MADRID, Hispania

RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez, ameripotiwa kuwa amesikitishwa na jinsi kocha Zinedine Zidane, alivyoshughulikia sakata la Bale wakati mshambuliaji huyo akiwa mbioni kujiunga na Tottenham Hotspur.

Bale aliwasili kwenye uwanja wa mazoezi wa Spurs juzi na anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Jose Mourinho kwa mkataba wa mkopo hadi mwisho wa msimu wa 2020-21.

Mchezaji huyo mwenye miaka 31 hakuwa na uhusiano mzuri na Zidane wakati wake huko Madrid, hadi kunyimwa nafasi ya kucheza katika hatua ya mwisho wa msimu wa 2019-20.

Kwa mujibu wa AS, Perez anaamini kwamba Zidane angeweza kumaliza tofauti yake na Bale, na rais akisisitiza kwamba Bale bado angeweza kuwa mali na msaada kwa klabu.

Taarifa zinadai kwamba Perez pia hakubaliani na Zidane juu ya Sergio Reguilon ambaye anatarajiwa kujiunga na Bale huko Tottenham msimu huu na mchezaji huyo wa miaka 23 alionekana kuwa wa ziada tu kwa mahitaji ya kocha wa Madrid.

Real wanatarajiwa kuwa na kifungu katika mkataba cha kumnunua tena Reguilon ingawa mabingwa hao wa La Liga wataruhusiwa kumrudisha Mhispania huyo huko Bernabeu baada ya miaka miwili.