NA KHAMISUU ABDALLAH

BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB), imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi ili kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei kiholela.

Ofisa Uhusiano wa bodi hiyo Badria Attai Masoud, aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya umuhimu wa kodi kwa wanafunzi wa skuli ya Sekondari Kidagoni Mkoa wa Kaskazini ‘A’ Unguja. 

Alisema, wanafunzi ni wadau muhimu na wana nafasi kubwa ya kuisadia serikali kuhakikisha inapata mapato yake kama ilivyokusudia.

Aidha alisema ZRB pekee haiwezi kukusanya mapato bila ya kushirikisha wadau wengine ambao ni wachangiaji wakubwa wa kodi.

“Nyinyi wanafunzi ni jeshi jengine ambalo tunaamini mtatusaidia katika kudai risiti pale mnapofanya manunuzi na kuwashajihisha wafanyabiashara kutoa risiti ili kutusaidia mianya ya upotevu wa mapato ya serikali,” alisema.

Ofisa Badria, alifahamisha kuwa wananchi wafahamu kuwa kodi inayokusanywa na bodi hiyo ndio inayotumiwa na serikali katika shughuli zake mbalimbali za kuleta maendeleo nchini ikiwemo huduma za elimu, afya miundombinu ya barabara na maendeleo mengine.

Alisema, Zanzibar ina rasilimali nyingi za ukusanyaji wa mapato hivyo wanafunzi kama wadau muhimu ni lazima kuhakikisha wanaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulipa kodi ambayo baadae inawarudia wenyewe.

Hata hivyo alisema, bado ZRB inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wimbi kubwa la wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kisheria, biashara ya magendo na wananchi kutodai risiti hali ambayo inapelekea upotevu mkubwa wa mapato.

Alisema kitendo cha wananchi kutodai risiti wanapofanya manunuzi na wafanyabiashara kutotoa risiti ni changamoto kubwa inayopelekea serikali kutokusanya mapato yake kama ilivyojipangia.

Hivyo, alisema ZRB itaendelea kuwaelimisha wananchi na wanafunzi wa ngazi zote hadi vyuo vikuu, ili kufikia ulipaji kodi wa hiari na serikali inapatikana mapato yake kwa wakati.

Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Bodi hiyo, Raya Suleiman Abdalla, alisema kodi ni tozo la lazima kwa wananchi kwani hakuna nchi inayoendeshwa bila ya kodi hivyo ni vyema wafanyabiashara kulipa kodi na kusajiliwa kihalali kwa mujibu wa sheria za kodi.

Hata hivyo, alisema lengo la utoaji wa elimu hiyo kwa wanafunzi ni kuielimisha jamii na kuona wafayabiashara wanalipa kodi kwa hiari na hawavunji sheria zilizowekwa.

“Ni imani yetu kuwa nyinyi wanafunzi mtaichukua elimu hii ili lengo letu la kufikia ulipaji kodi wa hiari kwa wafanyabiashara wetu unafikiwa na serikali yetu inapata mapato yake kama iliyokusudia,” alisema. 

Sambamba na hayo, alisema serikali imeweka bodi hiyo kuhakikisha inakusanya mapato na kuingiza katika mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya huduma mbalimbali za kijamii.

Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Makame Juma Badili, aliipongeza ZRB kwa uamuzi uliouchukua kuwapatia elimu hiyo ambayo walikuwa hawaifahamu kwamba mwananchi ni mchangiaji mkubwa wa kodi na kuomba kuendelea kutoa elimu hiyo mara kwa mara ili wanafunzi waweze kupata ufahamu juu ya umuhimu wa kodi.

Mwanafunzi Sleyum Issa Khamis, kwa niaba ya wananfunzi wenziwe waliahidi kuifikisha elimu hiyo kwa wengine na kuziomba taasisi nyengine kwenda kuwaelimisha ili wanafunzi waweze kujua mambo muhimu katika nchi.