NA MARYAM HASSAN
MAOFISA Rasilimali watu kutoka taasisi za serikali na binafsi wametakiwa kuzingatia wajibu wao ili kurekebisha mapungufu yanayojitokeza.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Kazi Zanzibar, Fatma Iddi Ali, wakati akifungua mafunzo kwa maofisa hao yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) yaliyofanyika katika ukumbi wa Uhuru, Kariakoo mjini Zanzibar.
Aliwataka kutambua kuwa wao ni viungo muhimu katika taasisi zao iwe serikalini au sekta binafsi huku akisisitiza kuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu kwa kazi wanazozifanya.
“Mafunzo mnayopewa nakuombeni mkayafanyie kazi kwa sababu ni nyenzo muhimu ili kuleta mabadiliko katika taasisi zenu,” alisema.
Akiwasilisha mada juu ya matumizi ya sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar, Mwanasheria Ramadhan Juma Suleiman alisema wafanyakazi wote wanapaswa kutii sheria ikiwa ni pamoja na kujisajili na kuwasilisha michango kwa wakati.
“Kusajiliwa kuwa mwanachama wa ZSFF (mfuko wa hifadhi ya jamii zanzibar) sio jambo la hiari bali ni lazima kila muajiri kuhakikisha anawasajili wafanyakazi wake na kuwasilisha michango yao kwa wakati,” alisema Ramadhan.
Afisa Mkuu wa usajili wa wanachama Rajab Haji Machano, alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni pamoja na kutokukamilisha vielelezo vinavyotakiwa wakati wa usajili.
Naye Mkuu wa kitengo cha mafao Zainab Rajab Baraka alieleza kuwa mfuko huo umeweka utaratibu wa kisheria kwa watumishi na wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi kupumzika baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu.
“Watumishi wote wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa na kuandaa taarifa zote muhimu zinazohitajika katika hatua ya maombi ya mafao yao,” alieleza.
Wakichangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika warsha hiyo, washiriki wa mafunzo hayo waliahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kuimarisha utendaji wa kazi zao.
Walisema mabadiliko ya taasisi zao yanahitaji ushirikiano kati ya watendaji na viongozi hivyo ni vyema wakashirikiana ili kupunguza malalamiko ya wananchi wanaokwenda kupokea huduma katika taasisi zao.