NA HANIFA SALIM

OFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, amewataka wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuitumia fursa iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) ili iwe ni ngazi ya kufikia malengo yao.

Aliyasema hayo wakati akifungua maonesho ya siku maalum kwa wanafunzi wapya wanaotarajia kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2020/2021 yaliyofanyika uwanja wa Gombani.

“Kupitia chuo chetu mwananchi atafahamu na atahudumiwa, tunaushukuru uongozi wa ZU kwa namna unavyotusaidia,” alisema.

Alieleza, serikali kupita wizara ya elimu ina uhusiano mzuri sekta binafsi za elimu ikiwa ni pamoka na chuo hicho.

Alisema vijana waliomaliza kidato cha sita kisiwani humo ni takribani 500, hivyo aliwataka kuitumia vizuri fursa ya uwepo wataalamu wa chuo hicho.

Mapema Mkuu wa Idara ya Utawala wa ZU, Dk. Rukiya Wakif Mohamed, alisema, lengo la maonesho hayo ni kukitangaza chuo pamoja na kozi zinazotolewa.