NA ASYA HASSAN

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imeandaa mikakati ya kudhibiti uingizaji na usambazaji holela wa huduma ya nishati ya gesi ya kupikia (LPG) hapa nchini.

Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Hassan Juma Amour, alisema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi hiyo Maisara wilaya ya Mjini.

Alisema miongoni mwa mikakati waliyoiandaa ni pamoja na kuwataka waingizaji wakubwa na wasambazaji wa jumla wa bidhaa hiyo kukata leseni ili waweze kutambulika kisheria na kuweza kuifanya biashara hiyo kihalali.

“Waombaji tayari weshaleta maombi yao, yamepitiwa na kuchunguzwa ili kujua kama watoa huduma hao wanakidhi matakwa, ambapo kazi hiyo tayari imekamilika na sasa wapo katika hatua ya matayarisho ya utowaji wa leseni hizo kwa waingizaji na wasambazaji hao,” alisema.

Alisema wameamua kufanya hivyo baada ya kubainika kwamba biashara ya gesi ilikuwa ikiendeshwa kiholela bila ya kuzingatia sheria na kanuni za nchi.

Aidha alifahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia kuifanya biashara hiyo kuingizwa na kuendeshwa kwa misingi ya usalama na viwango vinavyokubalika.

Ofisa huyo alisema sekta ya gesi ni sekta muhimu na inakuwa kwa hatua kubwa hivyo inahitaji kuwekewa usimamizi wa hali ya juu ili iweze kuendeshwa kisheria na kuepukana na athari.

Sambamba na hayo alisema wameamua kusimamia sekta hiyo kwa lengo la kuwafanya waingizaji na wasambazaji wa bidhaa hizo waweze kufuatia sheria na kanuni ili kuweza kuepusha athari mbalimbali zitakazoweza kujitokeza.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wafanyabiashara wanaoingiza na kusambaza biashara hiyo hapa nchini kufuata kanuni na vigezo vilivyowekwa na ZURA ili biashara hiyo iendeshwe kwa misingi ya usalama na viwango ili wananchi waweze kuridhika na huduma hiyo.

Akizungumzia bei ya mafuta ofisa wa Mamlaka hiyo Mbaraka Hassan Haji, alisema bei ya bidhaa hiyo kwa mwezi huu wa Septemba imepanda ukilinganisha na bei ya mwezi wa Agosti mwaka huu.