ADDIS ABABA,ETHIOPIA

UMOJA wa Mataifa umeripoti kuwa watu milioni moja wameathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Ethiopia, ambapo laki tatu miongoni mwao wamelazimika kuyahama makaazi yao.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilieleza kuwa, mvua kubwa zinazonyesha katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika zimesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kuwafanya watu takriban lakini tatu kuhama makaazi yao tangu mwezi Juni mwaka huu hadi sasa.

Aidha taarifa hiyo ilisema walioathirika zaidi na majanga hayo ya kimaumbile ni wakaazi wa majimbo ya Afar, Oromiya, Gambella, Kusini, Somalia na Amhara, huku ikionya kuwa, mafuriko hayo pia yaliharibu taasisi za afya na kumekuwa na uhaba wa dawa.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa,mazingira machafu yaliyosababishwa na mafuriko hayo yaliongeza hatari ya kukithiri kwa maambukizi ya virusi vya corona na ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema dola milioni 40 zinahitajika kwa ajili ya kuwafikishia misaada wahanga wa mafuriko hayo hasa chakula,dawa na nyumba za kuwasitiri.

Mbali na Ethiopia,nchi nyengine kadhaa za Afrika zikiwemo Niger, Sudan, Burkina Faso na Senegal zimekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tangu mwezi Juni mwaka huu,ambapo mamia walifariki dunia.