Alikuwa ni kiongozi wa kupigiwa mfano nchini, Afrika na dunia

Aliweka misingi imara na kupiga vita ubaguzi wa mambo yote

NA KAUTHAR ABDALLA

MIAKA 21 iliyopita siku kama ya leo Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liligubikwa na majonzi mazito kutokana na kifo cha mwasisi wetu na baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia Alhamisi majira ya saa 4:30 asubuhi kutokana na maradhi ya saratani ya damu katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London.

Watanzania na wapenda Demokrasia ya kweli, leo hii wanakumbuka kifo cha baba wa taifa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika taifa hili.

Pamoja na mambo mengine lakini Mwalimu Nyerere alipigania uhuru na ukombozi wa Taifa letu na nchi za bara la Afrika zilizokuwa zikitawaliwa na wakoloni pale ambapo tayari Tanganyika wakati huo ikiwa imeshapata uhuru wake mwaka 1961 na baadae kuungana mwaka 1964 na kuwa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Ni ukweli usiopingika kuwa Mwalimu aliweza kujenga umoja na mshikamano wa taifa kwa kuhimiza utu,upendo, haki na usawa, pamoja na kupiga vita ubaguzi wa aina zote unyonyaji, ukabila na udini.

Tanzania hivi sasa inayokisiwa kuwa na watu wapatao milioni 45 ambapo kuna makabila Zaidi ya 120 na dini tofauti hivyo kutokana na misingi aliyoiweka ni vigumu watu kubaguana kwa mambo hayo.

SIKU ambayo mwili wa Baba wa Taifa Mwl. Nyerere ulipowasili nchini kutoka Uingereza miaka 21 iliyopita mamia ya wakazi wa Dar –es Salaam walijipanga barabarani kutoka uwanja wa ndege.

Inapokosekana mizizi hiyo ni muhali mno kuondoa maadui wakubwa ambao ni ujinga, umasikini na maradhi ambayo ndio mambo makubwa yanayobomoa juhudi za kuendeleza maendeleo na kudumisha umoja wa taifa hili.

Hivyo hakuna budi kuwa na mitaala maalumu ambayo itaweza kufundisha namna ya Historia ya Tanzania sambamba nay ale yaliyokuwepo kabla na baada ya uhuru kupitia baba wa taifa mwalimu Nyerere.

Makundi kadhaa yanahitaji kupata historia ya maisha jinsi yalivyokuwa nyuma na namna maisha yanavyoendelea ambapo ukilinganisha na sasa kuna mambo mengi yanaweza kupatikana.

Kundi muhimu ambalo linahitaji kupata historia ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa la baadae hivyo kuna ulazima na umuhimu wa kuyajua mengi yaliyopita ikiwemo ya viongozi wao wa Kitaifa ambao wametangulia na wameshafariki.

Kwa upande mwengine tuseme kwamba vijana wengi hivi sasa hawajui historia za viongozi wao wa nchi waliotangulia pamoja na michango yao mikubwa iliyofanikisha maendeleo nchini.

Miongoni mwa viongozi ambao wanapaswa kujulikana historia ya maisha  ya uhai wao kwa vijana ni baba wa taifa Hayat Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume ambao kwa ujumla wao walijitolea muda wao mwingi katika kupigania mataifa yao na hatimae kupatikana taifa moja lenye nguvu ambalo kwa sasa tunajivunia utaifa wa Tanzania duniani kupitia marehemu hawa.

Yapo mambo mbali mbali ambayo yalifanywa na Mwalimu Nyerere katika uhai wake na yanapaswa kujulikana na vijana wa sasa ambapo Serikali kupitia Wizara ya Vijana ni muhimu kuona wanawapa elimu kuhusu maisha yake.

Historia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ina mambo mengi aliyoyafanya wakati wa uhai ambayo yamejikita katika Nyanja mbali mbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni lazima kuhakikisha vijana wanakuwa katika misingi ya historia ya viongozi wao waliotangalia imepanga kuwaeleza vijana maudhui ya filosofi ya Hayat baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jinsi alivyokuwa akiishi ili kuwafanya vijana wanatambua umuhimu wa jitihada zake zilivokuwa zikisaidia katika kuendeleza maendeleo ya nchi.

Mratibu wa vijana Shaame Sheha Haji, kutoka Idara ya vijana, amesema hatua hiyo itasaidia kuwafanya vijana kutambua na kumfahamu Nyerere katika jitihada zake za kutafuta maendeleo ya nchi.

Alisema vijana wanapaswa kuelezwa kuwa Mwalimu alikuwa anataka watu wawe huru,wafanyekazi pamoja na kusisitiza kuelimishwa kuishi katika mazingira aliyokuwa nayo.

“Ni ngumu katika miaka ya sasa kuona vijana wanaishi mazingira ambayo alikuwa akiishi Mwalimu Nyerere kwani mafanikio mengi ya kimaendeleo yaliweza kufikiwa kutokana na jitihada zake”, alisema.

Hata hivyo alisema tatizo kubwa linalojitokeza kwa vijana ni kutokuwa wazalendo wa nchi yao pamoja na kutomfahamu kwa undani kiongozi huyo, ambapo hawako tayari kujitolea katika shughuli za kijamii zinazoleta maendeleo na kusaidia kukuza uchumi wa nchi yao.

Wizara pia inakusudia kufanya program ya uzalendo ili kuwafanya vijana wajitolee kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuona umuhimu wa kitu hali ambayo itasaidia kuenziwa na kukumbukwa kwa jitihada zao walizozionesha.

Kuna mambo mengi ambayo aliyafanya Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake na yanapaswa kuekewa kumbukumbu pamoja na kuelimishwa vijana wa taifa la leo ili kuhakikisha kwamba mawazo na fikra zake zinaendelea kuwa hai.

Katika kuadhimisha siku hiyo pia Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tanzania Bara jumla ya vijana 100 watapanda mlima Kilimanjaro kwa awamu tatu ikiwa hadi sasa awamu mbili zimeshatekeleza bado moja ambayo itatekelezwa siku ya kilele na vijana 19 kutoka Zanzibar watashiriki.

Alisema upo umuhimu wa vijana kuendelea kutambua kuwa tunu za amani na umoja zilikuwa miongoni mwa falsafa kuu ya Mwalimu Nyerere ambapo matokeo yake ni umoja na mshikamano wa Taifa uliopo hadi sasa.

MAMA Maria Nyerere, mjane wa baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa katika moja ya misa ya kumbukumbu ya kifo cha mumewe katika kijiji cha Butiama ambapo viongozi wa dini waliongoza misa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Butiama mjini Musoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Jenista Mhagama alisema Baba wa Taifa alikuwa kiongozi mzalendo kwa nchi yake na aliyejali utu na usawa.

Alisema ni jambo zuri kuona vijana wakiendelea kuenzi falsafa zake ambapo kwa kiasi kikubwa wamechangia katika sula zima la kudumisha umoja na mshikamano wa Taifa.

Alisema Mwalimu Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja, mshikamano pamoja na misingi ya kuwa na uchumi wa kujitegemea.

Mwalim Julius Kambarage Nyerere alizaliwa April 13 mwaka 1922 huko Butiama Mkoa wa Mara, na kufariki tarehe kama ya leo Oktoba 14 mwaka 1999. Alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania, Nyerere alikuwa mwenyekiti wa Tanu na baadae CCM.

Mwalim Nyerere aliingoza Tanzania tangu mwaka 1961 hadi mwaka 1985, na kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa Mwalimu Kazi hii ndiyo ilimpatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la “Mwalimu.” Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiyari baada ya kutawala kwa muda mrefu.

Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.

Mbali na hayo Hayati Nyerere aliwaasa sana viongozi wa Tanzania kuhusu suali la kupiga vita rushwa, ambalo limekuwa changamoto kubwa.

Mbali na kukumbukwa na watanzania, mwalim Nyerere anakumbukwa pia na waafrika kote barani hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika. Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.