Imeandaliwa na Sheikh; Kamal Abdul-Mu’ty Abdul-Wahed

Mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu cha Kimisri

Dar es Salaam, Tanzania

SHUKRANI zote anastahiki kuabudiwa yeye Mwenyezi Mungu bwana wa ulimwengu wote na Mtume Muhammada SAW ni mjumbe wake.

HAKIKA Mtume (S.A.W.) alikuwa mfano bora katika hali zake zote hasa katika tabia yake njema, ambapo alikuwa mchamungu. Mtume (S.A.W.) alikuwa anasifika kwa tabia zake njema mpaka makafiri wenyewe walikuwa wanamwita “As-Sadiq Al-Az=miin” yaani aliye mkweli na mwaminifu.

Mwenyezi Mungu Alimsifu Mtume wake (S.A.W.) kwa kusema: {Na hakika wewe una tabia tukufu} [68/4], naye Bibi Asha alipiulizwa kuhusu tabia yake Mtume (S.A.W.) alisema: “Kwa hakika tabia yake zilikuwa ndizo Qurani” maana alikuwa na tabia zinazotokana na mafunzo ya Qurani Takatifu.

Kwa mujibu wa aliyoyasema Bi. Aisha tunaelewa kuwa tabia za Mtume (S.A.W.) ambazo kila mwislamu anatakiwa kuwa nazo ni tabia zailizoambatana na mafunzo na maadili ya dini hiyo adhimu kwa mujibu wa yaliyokuja katika Qurani Takatifu.

Tabia hizo ni nyingi hatuwezi kuzieleza kirefu katika makala moja, lakini kuna tabia zinazoongoza kama vile; upole, uaminifu, ukweli, uadilifu, ukarimu, rehma na huruma.

Kwa kuangalia sunna za Mtume (S.A.W.) tunatambua namna alivyokuwa Mtume wetu ni mfano bora wa mwenye tabia njema na watu wote na katika hali zote hakuwa na bughudhi wala chuki wala jeuri hata kidogo. Zaidi ya hayo Mtume (S.A.W.) alikuwa na hamu sana kuwafundisha maswahaba zake wawe na tabia njema na wanadamu wote mpaka maadui, isitoshe alikuwa anawausia wawe wapole na wanyama pia.

Vile vile, inafahamika kwamba ubora wa maisha ya waislamu unategemea kiwango walicho nacho kutoka tabia njema ambazo zina umuhimu mkubwa mno katika dini hiyo, mpaka Mtume (S.A.W.) alijumlisha malengo ya utume wake katika kauli yake: “Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema“. Tabia hizo ni kipimo cha kusanifisha jamii na kufanikiwa kwake, ambapo jamii bora ni ile inayofuata maadili ya kibinadamu na tabia njema baina ya watu wake kwa kusifika kwa sifa nzuri kama vile; ushujaa, ukarimu, ukweli, huruma, rehma, uaminifu, uadilifu n.k.

Kwa hivyo, tunatambua vipi dini yetu adhimu inategemea na kuzingatia sana tabia njema na maadili mema, mbali na visa vya Manabii na Mitume, tunaona Qurani Takatifu inatoa wito wa kutakasisha tabia na kuchunga maadili kwani ni sababu ya kutukuka kwa umma wowote. Mwenyezi Mungu Amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu,na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, nauovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka} [16/90]. Na tukifuatilia aya za Qurani Tukufu tutaelewa kuwa tabia njema ndiyo msingi muhimu wa umma wetu huu na hakuna dalili lililo wazi zaidi kuliko kumsifu Mtume kwa: {Na hakika wewe una tabia tukufu} [68/4]. Na kauli yake Mtume alipotaka kubainisha lengo kuu la utume wake: “Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema“.

Kwa upande mwingine, Qurani Tukufu ilituhadithia kuhusu hatima ya tabia mbaya na ukosefu wa maadili na sifa nzuri na namna ilivyokuwa hali hii sababu ya kuporomoka na kusambaratika kwa jamii na staaraabu nyingi duniani. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutendamaovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa} [17/16] na Qurani na Sunna imejaa visa vya umma zilizoangamizwa kwa sababu ya tabia zake mbaya, mifano ni kama vile; kaumu wa Manabii Hudu, Swaleh, Luut, Shuaieb na wengine ambao walichafuka kitabia wakastahiki kuadhibiwa duniani na adhabu ya akhera ni kali zaidi.

Aya nyingi katika Qurani zimesimulia visa vya umma hizo, kuhusu kaumu Aad Mwenyezi Mungu Amesema: {Ama kina A’di walijivuna katika nchi bila ya haki,na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi?Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawawanazikataa Ishara zetu! * Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika sikuza ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katikauhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera inahizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa} [41/15-16]

Na kuhusu kaumu wa Nabii Swaleh Mwenyezi Mungu Amesema: {Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha} [27/48] Ama kaumu Luut Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pale Lut’i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo * Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli * Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa!} [29/28-30]

Hali hiyo hiyo ilikuwa na kaumu wa Nabii Shueib kama ilivyosimuliwa katika Qurani Tukufu: {Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua’ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwishakufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini * Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi  Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na kumbukeni mlipokuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi} [7/85-86].

Hivyo ndivyo, mtazamo wa Uislamu kuhusu tabia njema na athari ya kuutekeleza katika hali halisi ya maisha ya walimwengu wote kwa jumla na hasa hasa waislamu na jamii za kiislamu.