NA ABOUD MAHMOUD

MABINGWA wa ligi kuu ya soka Zanzibar, Mlandege FC wamesema endapo watapata kucheza mechi za kirafiki na timu za nje ya Tanzania zinaweza kuwasaidia kufika mbali katika mashindano klabu bingwa Afrika.

Akizungumza na gazeti hili kocha mkuu wa klabu hiyo, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alisema kutokana na uzoefu wa nchi hizo kushiriki katika mashindano hayo yanaweza kuwasaidia kujua mbinu wanazozitumia.

“Hivi sasa tunaenda kucheza na ndugu zetu wa Simba hawa wana uzoefu mkubwa sana katika mashindano na tunaamini watatupa njia ambazo zitatusaidia sisi kufika mbali, lakini malengo yetu mengine kucheza na nchi jirani ambazo zitazidi kutujengea uwezo,”alisema.

Kiduu alisema wakipata timu kubwa kutoka nchi kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na nyengine, ambazo zipo vizuri kisoka wataweza kufahamu jinsi ya kwenda kucheza na timu pinzani.

Kuhusiana na kikosi chake Kiduu alisema kipo vizuri kwa ushindani kwani mazoezi wanayofanya pamoja na mechi za kirafiki walizocheza zinawapa matumaini.

Alisema tayari wamecheza mechi mbili ikiwemo ya ZFDC daraja la pili kwa kuwafunga magoli 5-0 na timu ya Chuoni ambayo walitoka sare ya goli 1-1.