BAKU, AZERBAIJAN

WATU wapatao saba wameuawa, baada ya kombora kuangukia kwenye nyumba kadhaa, katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Azerbaija wa Ganja.

Mashambulizi hayo, ambayo yamefanyika saa chache, baada ya kushambuliwa mji mkuu wa jimbo la Nagorno-Karabakh, Stepanakert, yanaashiria kuendelea kwa mapigano, kwenye mzozo wa wiki tatu sasa, baina ya Armenia na Azerbaijan.

Waandishi wa shirika la habari la AFP mjini Ganja, wameripoti kushuhudia majumba yakigeuzwa vifusi, huku watu wakikimbia huku na kule, na wafanyakazi wa huduma za uokozi, wanaendelea kusaka walionusurika.

Msaidizi maalum wa Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan, amesema zaidi ya nyumba 20 zimeharibiwa na mashambulizi hayo, huku watu wengine 10 waliuawa kwenye mji huo huo, kutokana na makombora.

Uturuki na Urusi, ambazo zinaunga mkono pande tafauti za mzozo huo, zimetowa wito wa kusitishwa mapigano.