NA TATU MAKAME

LEO Zanzibar inaadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) ambapo kwa kawaida huadhimishwa siku ya mwezi 11 mfunguo sita kwa mkesha wa Maulid yanayosomwa kitaifa kila mwaka.

Sherehe ya maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad yatasomwa katika viwanja wa Maisara Mjini Unguja na kuhudhuriwa na waumini wa dini ya kiislamu,wakiwemo walimu na wanafunzi wa madrasa mbalimbali, mashekhe na maimamu kutoka Zanzibar na Tanzania pamoja na viongozi wa chama na Serikali.

Maulidi haya yamesomwa kabla ya mwezi 11 uliozoeleka kutokana na serikali kuamua kufanya hivyo kufuatia uchaguzi mkuu ambao uko karibu kabisa na mwezi 12 mfunguo sita.

Kwa kuwa maulid ya kiongozi huyo wa kiislamu ni ya kipekee kwa nia njema kabisa kuyaweka katika kipindi hiki ni jambo la kuwafiki bila ya pingamizi ya aina yoyote.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa mufti wa Zanzibar Shekh Khalid Ali Mfaume, alisema sherehe hizo zimerejeshwa nyuma kutokana na kuingiliana na harakati za uchaguzi ambao utafanyika Oktoba 28 mwaka huu.

“Mwaka huu tutasherehekea siku ya uzawa wa Mtume mwezi Mosi mfunguo sita maana mwezi 11 itakuwa mkesha wa siku ya uchaguzi”, alisema.

Kusherehekea siku hiyo ni kukumbuka yale mambo mema yaliyoyaanzisha na kiongozi huyo ikiwemo kuwakumbusha waumini kuongeza ibada kama kuendeleza Sunna mbalimbali kwa kusoma Qurani na sala za sunna.

Hii inatokana kuendelea na kuenzi mema na mazuri yaliyofanywa na kiongozi huyo katika uhai wake pamoja na kuukumbusha umma uliobakia kuendeleza nyayo za kiongozi huyo katika kufanya mambo mema na kukatazana maovu.

Ni ukweli usiofichika kuwa sherehe za kuzaliwa kwa Mtume (S.A.W) zinapofanyika waumini hupata fursa ya hukumbusha mambo aliyoamrisha Allah (SW) na Mtume wake (SAW) na kucha yote aliyokataza kusudi waumini kusimamakatika nguzo ya kumpwekesha muumba wa ulimwengu wote.

Hivyo kwa kuwa mwezi huu ni miongoni mwa miezi mitukufu ya kiislamu, waumini wa kiislamu hawana budi kuzidisha twaa kusudi kwamba kujielekeza kwenye mambo mema yatakayomfaa mja akhera aendako.

Mtume wetu Muhammad aliyetumwa kwetu ameweza kuishi kwa kuzingatia maamrisho ya dini aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Aliweza kutekeleza masharti yote ya dini pasi na kuacha hata chembe kama alivyohusiwa na Mwenyezi Mungu.

Kufuatia mfumo wake wa maisha, Mtume wetu Muhammad ameweza kuwa mfano bora kwa jamii ya Waislamu na kuwakilisha dini ya Kiislamu kwa ujumla.

Dini ya Kiislamu imeletwa kwetu kikamilifu na kwa mifano bora kupitia Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye ana umuhimu mkubwa.

Yeye ni mtume aliyeishi kwenye jamii iliyokuwa imepotoka kwa ushirikina, ukafiri, na dhuluma na akaweza kuibadilisha na kuiweka kuwa katika mfumo wa maadili ya Kiislamu. Uwezo huo wa kuibadili umma huo unaweza kusemekana kuwa pia miujiza mengine baada ya Quran.