KWA miaka na dahari jamii yetu hapa Zanzibar imekuwa na utamaduni wa kusoma maulid karibu mwezi mzima wa mfunguo sita ambao ndio unaaminika aliozaliwa kiongozi wa dini ya kiislamu Mtume Muhammad (S.A.W).

Kusomwa maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), limekuwa jambo la kiutamaduni, kwani sehemu za vijijini kila kiambo kwa takriban mwezi mzima huwa na siku yake ndani ya mwezi huo kusomwa maulid.

Katika kisomo cha maulid, kikubwa kinachofanyika ni kuzitaja sifa za kiongozi huyo wa umma huu na waislamu hupata fursa ya kumswalia na kumtukuza kwa kumpa heshima anazostahiki kiongozi huyo wa dini.

Kama tulivyotangulia kueleza hapo awali, suala la kusomwa maulid, limekuwa la utamaduni wa muda mrefu hapa Zanzibar na waislamu hapa nchini wamelirithi kutoka kwa vizazi vilivyotangulia.

Hata hivyo, kadiri siku zinavyokwenda suala la kusomwa maulid limeanza kuwagawa waislamu hapa Zanzibar mapande mawili, kwani wapo wanaunga mkono na kuibuka kundi linalopinga kusomwa maulid.

Tunataka kuweka wazi na tueleweke vyema, sisi Zanzibar Leo si wataalamu tuliobobea kwenye masuala ya dini kiasi cha kutoa fatwa, lakini kwa tunavyoelewa suala la tofauti za kifkra katika uislamu (school of thought) sio jambo geni.

Utofauti wa kifikra (school of thought) upo katika uislamu kwa muda mrefu, kwa hivyo hatushangai leo kujitokeza wengine wakipinga kusoma maulid ya uzawa wa Mtume Muhammad (S.A.W), wengine kufikia hatua ya kuyaharamisha ama kuyaita bidaa.

Ni vyema tuwakumbushe waislamu kuwa kuhitilafiana kimawazo (school of thought), kwa wanazuoni wa zamani kulilenga kuinua dini, lakini pia historia inaonesha kuwa wanazuoni waliokuwa wakihitilafiana kimtazamo walikuwa wakiheshimiana sana.

Kinachotushangaza ni kuona hivi sasa hitilafu za kidini hasa kwenye suala la maulid na mambo mengineyo hazilengi kuijenga dini, wala hakuna kuheshimiana na badala yake zina mtazamo wa kuibomoa, huku kukiwa na kulazimisha kuamini hoja.

Kwa tunavyofahamu Mwenyezi Mungu , ametuamrisha katika kitabu kitukufu cha kur-ani tumswalie Mtume Muhammad (S.A.W), suali linakuja je! hawa wanaosoma maulid ambayo pamoja na mambo mengine wanamswalia Mtume je wanafanya makosa?

Kwa ushahidi huo wa kur-ani, tunadhani si vibaya watu kukusanyika kumswalia, kumsifu na kumtukuza Mtume Muhammad (S.A.W), kwa sababu wanaofanya hivyo wanatekeleza agizo la Mwenyezi Mungu. 

Kama yapo mambo ambayo yanakwenda kinyume kwenye utaratibu wa sasa wa kusoma kwa maulid, kwa mfano mchanganyiko wa wanawake na wanaume, haya yaelezwe wazi kuwa hayakubaliki.

Kwa ushauri wetu si vibaya kila mmoja kubakia kwenye msimamo wake, lakini kitu kikubwa na cha muhimu ni kwa kila mmoja kuhakikisha anaheshimu mawazo ya mwengine na sio kushindikiza.

Wanazuoni wa zamani waliokuwa wanapingana kwenye suala zima la dini hawakuthubutu hata siku moja kupanda majukwaani kutukanana, kushambuliana na kushutumiana.

Mtu mwenye elimu na ucha Mungu hawezi kuthubutu kuwatukana wenziwe, wala hawezi kubishana kwa makele kama vila anagomba. Dini busara na ulinganio unaombatana na hekuma na busara.

Lazima waumini watafakari na waone hakuna sababu ya kuendeleza hitilafu za kidini ikiwemo suala la maulid, anayeamini aamini asiyeamini si lazima, kitu cha muhimu ni kuheshimiana.