ILIONEKANA kama hatua ya ghafla kuchukuliwa na rais wa Marekani, Donald Trump pale alipoutangazia ulimwengu kwa kutumia mtandao wake wa twitter, kwamba nchi yake ipo tayari kuiondoa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi duniani nchi ya Sudan.

Nchi ya Sudan iliwekwa kwenye orodha ya Marekani ya mataifa yanayounga mkono ugaidi baada ya mashambulio dhidi ya kituo cha biashara cha kimataifa cha New York mnamo mwaka 1993.

Sudan ilimuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zikiangaliwa na Marekani kama nchi zinazofadhili ugaidi duniani. Mataifa mengine ni pamoja Iran, Korea Kaskazini na Syria ambayo bila shaka kwa sasa yanaendelea kuwemo kwenye orodha hiyo.

Marekani iliudhika zaidi na kuiweka Sudan katika orodha hiyo pale aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Al-Bashir kutangaza uhusiano na aliyekuwa kamanda wa kundi la kigaidi la Al-Qaida, Osama Bin Laden mwishoni mwa miaka ya 1990.

Kwa muda wa miezi kadhaa serikali ya mpito iliyoingia madarakani baada ya kutimuliwa madarakani jenerali Omar Hassan al-bashir, imekuwa kwenye mazungumzo na maofisa wa Mareakani kutafuta njia ya kuondolewa kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani.

Alipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita, waziri mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdouk moja ya vipaumbele alivyovitangaza ni kuhakikisha kwamba atachukua juhudi za kuhakikisha nchi hiyo inaondolewa kwenye orodha hiyo ya Marekani.

Hata hivyo, rais aliyeondolewa madarakani al-Bashir alifanya juhudi katika miaka yake ya mwisho ya uongozi kubadilisha siasa zake na kufuata sera za Marekani na washirika wake ili kulisafisha jina la Sudan iondolewe katika orodha hiyo, lakini hakufanikiwa.

Katika mikutano ya maofisa baina ya Marekani na Sudan kutafuta suluhisho hilo, kila upande ulijaribu kumbembeleza mwenzake ambapo mwishowe ilikubaliwa Sudan ilipe dola milioni 335 kama fidia kwa waathirika wa mashambulizi ya kigaidi na familia zao.

Trump alisema mara tu Marekani itakapopokea dola milioni 335 kama fidia ya Sudan kwa familia za waathirika wa mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani, jina la Sudan litaondolewa katika orodha ya tawala zinazounga mkono ugaidi.

Baada ya Sudan kukubali kulipa fedha hizo Trump, aliandika ndika kwenye mtandao wa Twitter, “hatimaye haki imepatikana kwa wamarekani na ni hatua kubwa kwa Sudan”.

Kuna taarifa kwamba tayari Sudan imeshaingiza mamilioni hayo ya dola kwenye akauti ya serikali ya Marekani, ambapo zitatumika kuwalipa fidia waathirika wa shambulizi hilo.

Suali linaloulizwa na watu wengi ni kwamba kwanini Sudan imekubali kubeba gharama kubwa za kutaka iondolewe kwenye orodha ya Marekani kuwa miongoni mwa nchini zinazofadhili ugaidi?

Serikali ya Hamdok imechukua hatua ya kutaka kuondolewa kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi kwa sababu ya kiuchumi ambapo nchi hiyo imekuwa katika hali mbaya.

Gharama za maisha nchini Sudan imepanda maradufu ambapo kuna tatizo la ukosefu wa ajira na kuongezeka umasikini, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya kimaumbile kama mafuriko na hivi sasa kuenea virusi vya corona ni mambo ambayo yameifanya Sudan ikabiliwe na matatizo maradufu.

Nchi hiyo ina ukosefu mkubwa wa chakula hususan ngano ambcho ndio chakula kikuu ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa watu milioni 9.6 nchini Sudan wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula.

Moja ya sababu ya kuondolewa madarakani kwa Omar al-Bashir kwa njia ya mapinduzi mwa mmoja uliopita ilitokana na kupanda gharama za maisha kwa wananchi na mwishowe kuandamana ambapo walisaidiwa na jeshi kumuondoa madarakani rais huyo.

Kwa upande mwengine, Marekani ina ajenda zake kufikia hatua za kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi ikiwemo kuishindikiza nchi hiyo ianzishe uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Waziri wa habari za Sudan, Faisal Mohamed Saleh aliwahi kunukuliwa akisema kwamba nchi hiyo inakabiliwa na shindikizo kubwa ianzishe mchakato wa kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano na Israel.

Katika mazungumzo ya hivi karibuni kati ya wawakilishi wa mazungumzo wa Marekani, Sudan na Abu-Dhabi, upande wa Marekani ulisema kuwa Sudan inapasa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, baada ya Khartoum kukubali kuburuzwa na Marekani kulipa fidia ya mamilioni hayo ya dola, haitakuwa na budi kukubali shinikizo la Washington la kuitaka ijiunge na mkumbo wa baadhi ya nchi za kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimeeleza kuwa moja ya sharti lililotolewa na Marekani ambalo Sudan imelikubali ni kwamba nchi hiyo lazima iwe na mahusiano ya kidiplomasia na taifa la kiyahudi la Israel.

Mnamo mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka 2020, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alifanya ziara nchini Uganda na kukutana na kiongozi wa baraza la utawala la Sudan, Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan.

Hata hivyo mkutano wa Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan na Netanyahu ulisababisha ghadhabu kwa wananchi wa Sudan ambapo tayari walitaka kiongozi wao huyo afunguliwe mashitaka kwa kutaka kuanzisha uhusino na Israel.

Sudan ina sheria inayopiga marugu nchi hiyo kuwa na mahusiano na Israel, ambapo katika hatua ya sasa ya makuliano ya kuondolewa kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi, haieleweki serikali ya Khartoum imejipanga kuwaeleza nini wananchi wa Sudan.

Sudan chini ya orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi inatumikia vikwazo vya kuchumi na matokeo yake ni kwamba, imezuiliwa misaada ya kifedha na mikopo kwenye mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, wananchi wa Sudan wamenukuliwa wakiipongeza sana serikali yao kwa kukubali kuwalipa fidia waathirika wa shambulio hilo.

Hoja wananchi hao ni kwamba endapo nchi yao itaondoshwa kwenye orodha hiyo itapiga hatua kubwa za kiuchumi ikiwemo kuvutia wawekezaji kutoka nje ya taifa hilo.