NCHI yetu inaamini kwenye usawa wa binaadamu na kwamba kila mwanadamu ana haki zake ambazo huzipata siku ya kwanza anapokuja duniani na zitamalizika siku yake ya mwisho ya kuondoka duniani.

Katiba ya Zanzibar na hata mikataba ya kimataifa imeeleza na kutoa ufafanuzi wa haki mbalimbali ambazo wanaadamu wanaweza kunufaika na haki hizo.

Ni jambo la faraja kwamba serikali na taasisi za kiraia zimekuwa zikihamaisha na kutoa elimu juu ya suala la haki za wananchi hasa wale wa makundi maalum wakiwemo walemavu.

Hata hivyo kuna mengi sana kwenye suala la haki za wananchi hasa wale walio kwenye makundi maalum wakiwemo walemavu, ambapo haki zao zimekuwa zikinyongwa.

Kiukweli kabisa jamii yetu imekuwa ina ujinga mkubwa tena ule wa kale, kuona hadi leo baadhi ya wanafamilia wanaendelea kuwaficha kwa kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu.

Haya ni mambo ya kusikitisha sana na tunathubutu kusema ni ujinga uliofanywa na kizazi cha kale, ambacho kilishindwa kuzingatia, kuzitetea na kuzitekeleza haki za watu wenye ulemavu, hali ambayo haiwezi kuzingatiwa katika maisha ya karne hii.

Katika kizazi cha kale wapo waliokwenda mbali zaidi kwa kufikiri kuwepo mlemavu katika familia ni chanzo cha mikosi na nuksi, hawana tofauti sana na kizazi cha sasa chenye mawazo potofu kinachoona haya kuwa na mtu mwenye ulemavu katika familia.

Unapodiriki kumficha mlemavu kwa kumfungia ndani, maana yake umemnyima haki yake ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo angeweza kuyajua kwa msaada wa kutanuka kwa sayansi.

Huwezi kuamini lakini kweli kabisa, msaada wa sayansi umewezesha walemavu wasioona kushona kwa uhakika kwa kutumia cherahani, kuandika kwa kutumia kompyuta, kusoma nakadhalika.

Unaposhindwa kumpa nafasi mlemavu maana yake unamuweka kwenye mazingira ya kumfanya kama sio mtu kamili, wakati huyo ni binaadamu mwenye haki zake tangu siku alipozaliwa.