NA MADINA ISSA

VIJANA wamehimizwa umuhimu wa kuhamasisha jamii kuchagua viongozi wenye dhamira ya kupambana na umasikini na kubuni njia mbalimbali zitakazoongeza kipato chao.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kikwajuni, Injinia Hamadi Yussuf Masauni, aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa taasisi ya Mimi na wewe, pamoja na kongamano la matajiri wapya kuelekea uchumi wa Bluu kongamano ambalo limefanyika katika ukumbi wa ZSTC Saateni.

Alisema, mtazamo wa kiongozi bora unaelekea zaidi katika kijali matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi, ili kuona wanaishi vizuri.

Alisema miongoni mwa kiongozi wenye vigezo hivyo ni Dk. Mwinyi, kwani vipaombele vyake ni kukuza uchumi kupitia sekta tofauti kama uvuvi wa bahari kuu na fursa za kilimo na mifugo.

Aidha, aliomba taasisi ya Mimi na Mwinyi, kuhakikisha ushindi wa wagombea wa Chama cha Mapinduzi, ili kuona wanafikia malengo yao.

“Vijana hakuna sababu ya kutomchagua mgombea Dk. Mwinyi, kwani amekuwa akifanya kampeni zake kwa staili yake na kistarabu ya Hali ya juu, ikiwemo kujua changamoto zinazowakabili watu katika makundi mbalimbali” alisema.

Akitoa mada katika kongamano la matajiri wapya kuelekea uchumi wa bluu, mkufunzi Hassan Ibrahim, alisema, kunahitajika sera na sheria madhubuti zitakazoteengeneza uhalali wa fursa za ajira kwa vijana ambao kwa sasa wanaendelea kusomea fani mbalimbali.

Nao washiriki wa Kongamano hilo, wamewataka vijana wenzao kutambua kuwa dhamira na mipango ya vijana itaweza kutekelezeka endapo nchi itaendelea kuwa na amani kwa kukichagua Chama cha CCM.

Akifunga kongamano hilo, Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, alisema serikali imeandaa miundombinu ya kisasa kwa ajili ya uzalishaji, hivyo aliwataka vijana kujiendeleza kielimu, ili kuweza kukabikiana vyema uchumi wa Buluu.