NA ZAINAB ATUPAE

TIMU ya KVZ  FC  inayoshriki ligi kuu ya Zanzibar  inatarajia kushuka dimbani leo  kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Azam FC  kwenye uwanja wa Chamanzi Jijini Dar es Salaam.

KVZ ni mabingwa wa kombe la wa FA  2019-2020, ambao wanajiandaa kwa ajili ya mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika pamoja na ligi kuu ya Zanzibar.

Akizungumza na gazeti hili msemaji wa timu hiyo Said Salim Hazad,alisema  mechi hiyo itachezwa majira ya saa 1:00 siku.

Msafara wa timu hiyo umeondoka na  wachezaji 18 pamoja na viongozi 10, baada ya kumaliza mechi hiyo siku ya pili watarudi kisiwani Unguja kuendelea na majukumu yao mengine.

Alisema  tayari wamecheza mechi mbili za kirafiki na timu ya KMC na kupokea kichapo cha mabao 2-0,mechi na timu ya Ruvu Shooting walitoka sare ya kutokufungana.

“Tulikuwa hatuna lengo la kurudi huku tulitaka tumalize mechi yetu  na Azam FC ndipo turudi Zanzibar,lakini  ilitulazimu kurudi kukamilisha masuala ya paspoti za wachezaji  kwa ajili ya mashindano ya kimataifa,”alisema.

Kwa upande wake kocha  mkuu wa timu hiyo Sheha Khamis,alisema  lengo la kucheza mechi hizo mara kwa mara, ni kuwapa uzoefu wachezaji ,ili kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa pamoja na ligi kuu ya Zanzibar.

“Tunakwenda kucheza siku moja ya pili tunarudi tunasubiri mchezo wa ngao ya jamii  kati yetu na Mlandege, na taarifa ambayo tuliipata inatarajiwa kupigwa Novemba 1”alisema.