WANANCHI wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, mnamo Oktoba 28 mwaka huu watakwenda kwenye vituo vya kupiga kura kuchagua viongozi watakaodumu madarakani kwa miaka mitano.

Uchaguzi wa Oktoba 28 kwa Zanzibar utatanguliwa na zoezi la upigaji kura ya mapema, ambayo itapigwa na makundi maalum ya watu mnamo Oktoba 27 mwaka huu.

Ni kweli zoezi la kura ya mapema ni jipya kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambapo kwa mara ya kwanza linafanyika, hata hivyo zoezi la namna hii sio jipya katika nchi za wenzetu zinazoitwa zimekomaa kidemokrasia.

Kwa mfano Marekani ambayo mwaka huu nayo inakabiliwa na uchaguzi utakofanyika Novemba 3 mwaka huu, hadi mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2020 tayari watu zaidi ya milioni 4 walikishwa piga kura mapema.

Tunaeleza haya ili Zanzibar tusionekane sisi ni watu wa vituko kwa kuanzisha zoezi la mapema, ambapo baadhi ya wanaolilalamikia wanaelewa fika kwamba hili si zoezi jipya katika nchi za wenzetu.

Suala la uchaguzi wa awali Zanzibar ni la kisheria ambapo kwa mujibu sheria nambari 4 ya mwaka 2018 kifungu cha 82(1) na (2) kimefafanua vyema jinsi kura hiyo itakavyopigwa na watu wanaohusika na zoezi hilo.

Zoezi hilo la upigaji kura ya mapema ambalo lipo kisheria, kwa hakika linaonekana kupewa tafsiri mbaya linatiwa sumu hasa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa ambao wanaangalia maslahi yao zaidi.

Wapo baadhi ya wanasiasa wanalingalia zoezi kama limelenga kutoa upendeleo kwa baadhi ya vyama vya siasa, wanasiasa hawa ni wale wenye mitazamo miyepesi na wenye maslahi binafsi.

Wanasiasa hao wanadhania suala upigaji kura ya mapema limechomekwa kinyemela na Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kuwabeba na kuwasaidia wagombea wa baadhi ya vyama vya siasa.

Kinachotushangaza ni kwamba baadhi ya wanasiasa wanaoipinga kura hiyo ambayo imetolewa muongozo katika kanuni ya uchaguzi ambapo wadau wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa vilishiriki maandalizi na hatimaye kusaini makubaliano.

Kwa mujibu wa ZEC, kura ya mapema itapigwa na vikosi vya ulinzi na usalama, lakini sio kila askari atapata nafasi hiyo, bali wale watakaoshiriki kwenye zoezi la ulinzi siku ya uchaguzi.

Pia zoezi litawahusu wafanyakazi wa Tume hasa ikizinagtiwa kuwa siku ya Oktoba 28 wafanyaakazi hao watakuwa ndio wasimamizi wa kubwa wa zoezi zima la upigaji kura.

Unapopinga kura hii isipingwe maana yake unasababisha watu wengine kukosa haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Kwa mfano askari polisi ambaye amepangiwa kazi kituo cha kura kilichopo wilaya ya Kaskazini ‘B’, lakini yeye mwenye amejiandikisha kura kwenye kituo cha magharibi ‘B’, atapata muda kweli kwenda kupiga kura wakati analinda kituo cha kazi?

Kwani kuna hofu ya nini wakati zoezi la kura ya mapema litapigwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zote ikiwemo suala la vyama kuwa na mawaka kwenye vituo vya upigaji kura?

Huko tunakokwenda tunadhani Tume ifikirie kutanua wigo wa kuongeza makundi ya watu watakaopiga kura ya mapema wakiwemo waandishi wa habari, madaktari na kada nyengine.

Wapo wanasiasa wanahamasisha wananchi wajitokeze kupiga kura Oktoba 27, tunawaeleza kuwa hiyo ni kwa ajili ya siku maalum, hivyo ukijitokeza unavunja sheria.

Kama huhusiki kwenye zoezi la Oktoba 27 chondechonde usiguse kwenye kituo na kwamba wanaokushawishi wanalengo la kukuweka kwenye matatizo.