NA ABOUD MAHMOUD

WAWAKILISHI wa Zanzibar katika kombe la klabu bingwa Afrika na lile la Afrika Mashariki (Kagame) timu ya Mlandege FC, wamesema mechi yao ya kirafiki waliocheza na Simba imewapa njia ya kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Akizungumza na gazeti hili kocha mkuu wa klabu hiyo, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alisema lengo la kucheza mechi ya kirafiki na Simba ni kufahamu mbinu za mechi za kimataifa na kwa hilo wamefanikiwa.

Alisema ingawa katika mtanange huo walifungwa mabao 2-1 lakini imewapa njia ya kujifunza namna gani ya kucheza katika mashindano hayo hususan wakiwa ugenini.

“Tumecheza na Simba na wametufunga mabao  2-1 lakini lengo letu lilikua kwenda kujifunza mbinu za uchezaji wakati tukiwa ugenini na Alhamdulilah tumefahamu,”alisema.

Kiduu alieleza kwamba katika mechi hiyo, katika kipindi cha kwanza hawakufanya vizuri lakini mara baada ya kuanza kipindi cha pili walibadilika na kupata bao moja.

 “Tumeweza kufahamu mechi ya ugenini inachezwaje na nyumbani inachezwa vipi tunaishukuru sana klabu ya Simba tumekwenda kwa kujifunza na mafunzo tumeyapata na matumaini yetu kufanikiwa,”alieza Kiduu.