NA SAIDA ISSA, DODOMA

JESHI la Polisi Nchini Tanzania, limewataka waandishi wa habari nchini  kuandika habari za kweli zinazohusu uchaguzi mkuu na kutoka kwenye vyanzo sahihi vya habari, ili kujiepusha na kutoa habari za uongo.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania, Kamanda David Misime, kwenye uzinduzi wa kamati ya kitaifa ya uratibu na maridhiano kati ya jeshi la polisi na vyombo vya habari nchini humo.

Kamanda Misime, alisema wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu waandishi wa habari wanatakiwa kujiepusha na kuandika habari zinazoegemea upande mmoja na badala yake waandike habari zenye manufaa kwa Taifa.

“Msiandike habari zinazolenga mtu mmoja hakikisheni kuwa mnapoandika habario zenu zilenge Taifa kwa ujumla na siyo kumshambulia mtu mmoja,

“Hakikisheni kuwa habari mnazoandika kuhusu uchaguzi mkuu zinatoka kwenye vyanzo sahihi vya habari hizo ambavyo ndivyo vyenye mamlaka kisheria na si kuandika habari ambazo hazina ukweli zinazohatarisha usalama wa Taifa,” alisema Misime.