NEW DELHI, INDIA

MAHAKAMA  moja ya India imewaacha huru washitakiwa wote 32 wa uhalifu katika shambulio la mwaka 1992 la kuvunja msikiti uliojengwa katika karne ya 16.

Tukio hilo lilizusha ghasia kati ya wahindu na Waislamu na kusababisha watu 2,000 kuuwawa.

Viongozi wanne waandamizi wa chama tawala cha Hindu Nationalist Bharatiya Janata,BJP, ni miongoni mwa washitakiwa katika kesi hiyo ambayo ilifanyika katika mfumo wa sheria wa nchi hiyo wenye mwendo wa taratibu mno kwa karibu miaka 28.

Washitakiwa 17 kati ya 49 walifariki kwa kifo cha kawaida katika kipindi cha kesi hiyo.

Viongozi hao wanne wa chama cha BJP walishitakiwa kwa kutoa hotuba za uchochezi ambazo ziliwachochea mamia kwa maelfu ya wafuasi wao ambao walifunga kambi nje ya mji wa Ayodhya kabla ya kufanya shambulio hilo dhidi ya msikiti.