NA KHAMISUU ABDALLAH

HAKIMU Suleiman Said Suleiman, wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe imemuachia huru Yahya Ramadhan Ali (21) mkaazi wa Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akisoma hukumu kwa mshitakiwa huyo, alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kosa la kuvunja kutokana na ushahidi PW3 ulikuwa unagongana wenyewe na unatia shaka.

Hakimu Suleiman, alisema pia upande wa mashitaka umeshindwa kuonesha umiliki halali wa vitu vilivyoibiwa kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani kujionesha wazi yupi mmiliki wa vitu hivyo.

Mahakama baada ya maelezo hayo, ilisema kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kosa na kuamua kumuachia huru mshitakiwa huyo na ilitoa haki ya rufaa kwa siku 30 kwa mtu asieridhika na hukumu hiyo.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mohammed Haji Kombo, ulidai kuwa kesi hiyo, ipo kwa ajili ya kutolewa hukumu kwani upande wa mashitaka umeshamaliza kuwasilisha mashahidi dhidi ya mashitaka yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Ilidaiwa mahakamani hapo awali mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na mashitaka mawili tofauti ikiwemo la kuvunja nyumba mchana kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi kinyume na kifungu cha 296 (1) (2) na cha 297 (1) (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa Machi 11, mwaka 2017, saa 9:00 mchana huko Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mshitakiwa huyo alidaiwa kuvunja na kuingia kwenye nyumba ya Mwajuma Issa Mohammed, kwa lengo la kufanya kosa la wizi.

Hati hiyo, pia ilidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la wizi kinyume na kifungu cha 267 (1) na cha 274 (1) vya sheria ya makosa na adhabu namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.