NA ABDI SULEIMAN

MENEJA kampeni za Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Aboud Mohamed, amewaomba wananchi wa jimbo la Ole Wilaya ya Chake Chake, kuitumia bahati ya kipekee ya kupata viongozi wenye nia ya kuwatumikia wananchi.

Alisema jimbo la Ole katika miaka mingi lilikuwa chini ya utawala wa CUF, huku wananchi wakikosa maendeleo.

Alisema  hayo wakati akiwanadi wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani wa jimbo hilo, katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Vumba Vitongoji.

Alisema wananchi wa jimbo la Ole wana kila sababu kuwachagua wagombea wa wote wa CCM, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili wawaletee maendeleo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Ali Khalfan, aliwaomba wananchi kutokufanya kosa Oktoba 28, kwani wananchi wanahitaji maendeleo.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, alisema wananchi wa Ole wanahitaji maendeleo na vijana ndio viongozi wanaotarajiwa kuongoza nchi.