NA ASIA MWALIM

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Kamishna wa Polisi , Awadh Juma Haji, amesema mtu mmoja amefariki dunia akiogelea katika pwani ya Mazizini Unguja.

Kamanda akizungumza na Zanzibar Leo, huko ofisini kwake Mwembemadema Unguja, ambapo alisema marehamu huyo alijulikana kwa jina la Anuar Juma Seif  (16) mkaazi wa Kilimani Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alieleza kuwa marehemu kabla ya kifo chake alifika pwani akiwa na marafiki zake kwa ajili ya kuogolea, wakati wanaongelea alizidiwa na  maji na kupelekea kuzama pia kukosa hewa hadi kupelekea kifo chake.

Alisema tukio hilo lilitokea Oktober 3, mwaka huu majira ya saa 12:45 jioni huko mazizini wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa mjini magharibi Unguja, ambapo baada ya tukio hilo mwili wa marehemu ulikabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.

Aidha katika tukio jengine Kamanda alisema Jeshi hilo linaendelea kumtafuta dereva wa gari aliegonga na kusababisha kifo cha Justine Joseph Jonas (45) mkaazi wa Ng’ambo Wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kamanda Awadh, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 5, mwaka huu majira ya saa 12:30 jioni huko Bububu Kibweni Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema marehemu kabla ya kifo chake alikua akiendesha pikipiki aina ya sanleg rangi nyekundu yenye nambari za usajili Z 915 JQ akitokea upande wa Bububu Skuli kuelekea kwa Kisasi, aligongwa na gari isiyojulikana mmiliki wala nambari za usajili kwani bada ya tukio muhusika alikimbia na gari hiyo.