NA ABOUD MAHMOUD

WANANCHI wa Jimbo la Malindi wametakiwa kumchagua mgombea Uwakilishi wa Chama cha Wakulima AFP, ili awaondoshee changamoto zinazowakabili ikiwemo maji safi na salama.

Hayo yalisemwa na mgombea huyo, Hafidh Othaman Jabu ‘Bozo’ wakati akiomba ridhaa ya wananchi wa jimbo hilo nyumba kwa nyumba katika mitaa ya Gulioni, Mlandege, Mwembetanga na Mchangani.

Hafidh alisema imekua kilio cha siku nyingi kwa wananchi wa jimbo hilo kukosa maji safi na salama na kutumia maji ya chumvi yanayotokana na visima vilivyochimbwa  katika maeneo hayo.

Mgombea huyo alisema mara baada ya kupata ridhaa za wana Malindi hilo litakua jambo la mwanzo kwake kuhakikisha anawafanyia wananchi wake.

“Mimi nimezaliwa katika mtaa huu na sikukumbuki kunywa maji ya chumvi, lakini hivi sasa wananchi tunatumia kwa kuwa hakuna maji mengine, nakuhakikishieni mkinipa kura tatizo hili litakua ndoto,”alisema.

Aidha mgombea huyo, alisema wananchi wa Jimbo hilo wakimchagua atatumia mfuko wa Jimbo kuhakikisha anawatunza wazee kwa kuwapa huduma muhimu ikiwemo afya pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya kuwasaidia ili kujikwamua kimaisha.

Pia alisema atahakikisha anatumia fedha za mfuko wa Jimbo kuwasaidia vijana ambao wana dhamira ya kuendelea na masomo hususan  chuo kikuu ambao hawana uwezo wa kujisomesha.