BLOEMFONTEIN, AFRIKA KUSINI

AFRIKA KUSINI imefungua tena safari za anga za kimataifa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani miezi sita,ikigusia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya kila siku ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona.

Hatua hiyo ilianza Alhamisi,Nchi hiyo ilifunga mipaka yake mwezi Machi ikiwa ni sehemu ya hatua za kukabiliana na virusi vya corona.

Wasafiri wanaowasili kwa ndege kutoka nje ya nchi, watatakiwa kuwasilisha matokeo ya vipimo yaliyotolewa kabla ya safari, yanayoonyesha kuwa hawana virusi vya corona.

Watalii bado wanazuiliwa kutoka kwenye nchi zaidi ya 50 ambako maambukizi bado yapo juu, zikiwemo Marekani na Brazil.

Kufunguliwa huko kunatarajiwa kusaidia kuongeza shughuli za kibiashara ndani ya Afrika Kusini, nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika.

Ndege kutoka Ujerumani, Kenya na kwingineko ziliwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa katika jiji kubwa zaidi nchini humo la Johannesburg Alhamisi.