NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA ya Wilaya Mwera imemhukumu mshitakiwa Mawia Haji Mawia (37) mkaazi wa Ndagaa kulipa faini ya shilingi 8,000, na iwapo atashindwa atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mienzi sita.

Hakimu Rauhia Hassan Bakar, Kabla ya kutoa adhabu hiyo mshitakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu hana uwezo wa kumudu adhabu atayopewa.

Mapema wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Shumbana Mbwana, aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

alisema adhabu itayotolewa mahakamani hapo itasaidia kupunguza tatizo la wizi wa mazao katika mkoa wa Kusini Unguja.

Mawia alidaiwa kutenda kosa hilo Julai 24, mwaka jana majira ya saa 12:00 za jioni huko Kiboje wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo bila ya halali na kwa nia ovu alijimilikisha nazi sita zenye thamani ya shilingi 4,000, mali ya Idrissa Mtumwa Mkanga jambo ambalo ni kosa kisheria.

Baada ya kupewa adhabu hiyo mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo na kupelekea kupelekwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.