CASABLANCA, Morocco
AL Ahly imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele dhidi ya Wydad Casablanca baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa nchini Morocco.


Ahly iliwashangaza wenyeji kwa goli la mapema kunako dakika ya nne jijini Casablanca wakati Magdy Afsha alipoipita safu ya ulinzi na kuwaweka mbele miamba hiyo.


Wydad walipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha wakati walipozawadia mkwaju wa penalti kabla ya mapumziko ambapo shuti kali la Badie Aouk lilipookolewa na kipa wa Ahly, Mohamed El-Shennawy.
Wageni kisha wakazidisha uongozi wao katika kipindi cha pili huku mchezaji wa kimataifa wa Tunisia, Ali Maaloul, akifunga kwa mkwaju wa penalti.


Ahly ambao wameshinda taji mara nane, sasa wapo katika nafasi nzuri ya kutinga fainali kuelekea mchezo wa pili huko Alexandria wiki ijayo.
Kocha, Pitso Mosimane alichukua jukumu la kuinoa Al Ahly mwanzoni mwa mwezi, akitokea kuiongoza Mamelodi Sundowns kutwaa taji la ligi nchini Afrika Kusini.


Huo ulikuwa mtihani wa kwanza kwa kocha mpya wa Ahly, Mosimane baada ya ushindi mara mbili na sare kwenye Ligi Kuu ya Misri tangu alipochukua nafasi ya Uswisi, Rene Weiler.
Mechi nyengine ya nusu fainali ilitarajiwa kuchezwa jijini Casablanca jana kati ya mabingwa wapya wa Morocco, Raja Casablanca na Zamalek ya Misri.