NA MARYAM HASSAN
MAHAKAMA kuu Vuga imemhukumu mshitakiwa Sleveta Robert Mashada (42) mkaazi wa Paje kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwa kwa makusudi.
Hukumu hiyo, imetolewa na Jaji Rabia Muhammed, baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo na kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Jaji Rabia, amesema adhabu aliyoitoa itakua fundisho kwa wale wote wanaoshindwa kudhibiti hasira na kupelekea vifo vya makusudi.
Alisema mshitakiwa anyongwe hadi kufa na adhabu hiyo itawashikia wale wote wanaoshitakiwa kwa makosa ya aina hiyo.
Awali mshitakiwa inadaiwa kutenda kosa Hilo Agosti
10 mwaka 2013 majira ya saa 4:30 asubuhi huko Paje wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa huyo inadaiwa kwamba kwa makusudi na bila ya halali alimshambulia Maryam Hassan Ali, kwa kumpiga mapanga kichwani na mikononi wakati akiwa katika harakati zake za ujasiriamali wa kupiga tanu ya makaa na kusababisha kifo chake.
Kesi ilifunguliwa January 9 ya 2014 huku hatua ya pili ilifunguliwa Agosti 10 mwaka 2016 na kuanza kusikilizwa ushahidi Septemba 3, 2019.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Ali Yussuf ,aliiambia Mahakama kwamba yupo tayari kwa ajili ya kutolewa adhabu kwa mshitakwia huyo.