WASHINGTON, MAREKANI

SHIRIKA la kutetea haki za binadamu (Amnesty International), limeeleza juu ya wasi wasi mkubwa lilionao kutokana na kushamiri vitendo vya ghasia, machafuko na mapigano katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani.

Taarifa ya Amnesty International ilisema, kati ya mwezi Mei na Septemba mwaka huu, asilimia 75 ya mikutano ya kampeni za uchaguzi huko nchini Marekani imeshuhudia machafuko na mapigano baina ya makundi hasimu ya kisiasa.

Shirika hilo la Msahama Duniani lilisema kinachochochea machafuko hayo katika mikusanyiko hiyo ya kisiasa nchini Marekani ni uwepo wa raia waliojizatiti kwa silaha na kwamba waandamanaji na wapiga kura nchini humo hawana dhamana ya usalama wao.

Haya yanaripotiwa huku zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani kufanyika tarehe 3 ya mwezi ujao wa Novemba.

Wadadisi wa mambo wameonya kuwa, yumkini Marekani itashuhudia machafuko makubwa ya baada ya uchaguzi.

Wiki iliyopita, maafisa wa jimbo la Massachusetts nchini Marekani walitangaza habari ya kutokea mapigano kati ya waungaji mkono na wapinzani wa Rais Donald Trump katika mji wa Boston jimboni hapo.

Trump alikuwa akiunga mkono kila mara vitendo vya fujo na utumiaji nguvu vinavyofanywa na wafuasi na waungaji mkono wake wakuu, ambayo ni makundi ya wazungu wanaojiona bora kuliko watu wa asili nyingine, kwa ajili ya kushambulia maandamano ya wananchi wanaompinga.