NA MWANAJUMA MMANGA

KIKOSI cha doria cha Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka kimefanikiwa kumkamata Hatib Hassan (45) mkaazi wa Bungi akichimba mchanga katika maeneo ya serikali huko Bungi, wialya ya Kati Unguja.

Akizungumza na gazeti hili, Msimamizi wa sheria Maliasili, Madini na Misitu, Haji Haji Hassan, alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na gari ya ng’ombe na ng’ombe wake majira ya saa 12:00 asubuhi.

Alisema kijana huyo alikutwa akichimba mchanga huku akijuwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria ya mazingira.

“Uchimbaji wa mchanga huu ni kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria kwani hauna kibali na ndipo, tulipomkamata tulimtaka mtuhumiwa huyo kulipa faini ya shilingi 700,000 na baada ya kushindwa atapelekwa mahakamani,” aliongeza Haji.

Alisema pamoja na jitihada wanazozichukua, bado wananchi hawatii sheria na kuharibu maliasili ya mchanga yakiwemo maeneo ya fukwe za baharini na kuwataka wananchi kuzitumia vyema rasilimali za misitu kwa mujibu wa sheria.

Alisema uharibifu wa mazingira bado upo katika maeneo mengi ya Zanzibar, hivyo alihimiza haja ya kutumiwa vyema rasilimali hiyo, kwani zinaweza kumalizika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.