Ni za mabinti wao waliobakwa, kupewa ujauzito na baba zao

NA MWAJUMA JUMA

LICHA ya juhudi kubwa zinazochukuliwa kupinga vitendo vya udhalilishaji bado vitendo hivyo vinaendelea kutokana na baadhi ya watu hasa wanawake kuficha matukio hayo, kwa kuhofia talaka.

Wanawake pamoja na kuwa ni walezi wakuu lakini bado wanaonekana kutowatendea haki watoto wao mara tu wanapofanyiwa vitendo hivyo.

Kama ambavyo inavyojuulikana kwamba matendo hayo wafanyaji hao wanakuwa wamo ndani ya familia ikiwemo baba, kaka, wajomba na hata majirani lakini inakuwa ni vigumu kwa badhi yao kuwafichuwa.

Kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kubakwa lakini watoto hao wanashindwa kupata haki baada ya baadhi ya wazazi wao kuwafichia.

Katika makala hii imegunduwa kwamba sababu kubwa ambayo inaonekana kwa akina mama hao kuficha matendo hayo ni kuhofia kupewa talaka na waume zao.

Wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja wakizungumzia suala hilo  walionekana kukerwa sana na tabia hiyo ambayo waliisemea kuwa inawanyima haki watoto.

Walisema tabia ya wanawake hao kukaa kimya na kuyaficha matendo hayo kwa kuhofia talaka ni kosa kubwa na linafanya idadi ya watoto wao kufanyiwa vitendo hivyo kuongezeka siku hadi siku.

Wakizungumza katika mkutano wa wazi uliofanyika huko Kitope mkoani humo walisema wanawake wengi wamekuwa wakificha matukio ya udhalilishaji wanayofanyiwa watoto wao kwa kulinda ndoa zao.

Asya Fadhil Makame alisema kuwa pamoja na kuwa wanalinda ndoa zao lakini kuna mambo mengine hayapaswi kuvumiliwa na kuachiwa kwa sababu kuyaachia kwake kunamfanya mtoto kukosa haki yake.

“Kuna mambo mabaya hufanyiwa watoto wetu lakini eti kwa kuogopa talaka utamkuta mama ananyamaza hajui kama anavyofanya hivyo ni moja ya kuyafanya yazidi kuongezeka na kunyima haki za watoto wetu”, alisema Asya.

Alifahamisha kwamba ni wakati sasa kwa kila mzazi kuhakikisha wanawafichuwa watu wa aina hiyo hata awe nani ili kukomesha tabia hiyo.

“Tunafahamu kuwa mume ana nafasi yake katika ndoa lakini vitendo ambavyo huwafanyia watoto wetu havipaswi kufumbiwa macho, lazima tuyafichuwe ili watoto wetu wapate haki”, alisema Asya Fadhil.

“Tunapoendelea kunyamaza ndio tunasema kwamba tunataka haya matendo yaendelee”, aliongeza kwa hasira Fatma Suleiman.

Alisema kuwa ukiwa kama mzazi wakati mwengine unapaswa uwe na moyo wa ujasiri wa kuyatoa hadharani pasipo na kuhofia kitu.

Alifahamisha kwamba wanawafichia makosa yao watu ambao hawastahili, kwani kama kweli anaipenda familia yake ni lazima angaliona utu na kutofanya.

Alieleza kama mwanamme anataka kukuacha hata kama utamfichia utajikuta mwisho wa siku anakuacha na kubakia na majuto ambayo kwa kiasi kikubwa yanakuwa yanabakia kukuumiza kichwa.

Naye Mama mmoja (jina linahifadhiwa) mkaazi wa Kijichi, alikataa kutoa ushahidi baada ya mtoto wake kupewa ujauzito na mumewe ambae ni baba wa kambo.

“Nikisimama kutoa ushahidi mumewangu akifungwa atanihudumia nani, jambo hili sifanyi kabisa”, alisema huku akijua kama ni kosa kufanya hivyo lakini anahofia kuvunjika ndoa na kukosa huduma kama mumewe atafungwa.

Kwa upande wake mwanaharakati Hadia Ali Makame alisema kuwa imefika wakati akinamama kubadili mitazamo yao juu ya kuwalinda waume wao ambao huwafanyia udhalilishaji watoto wao ili kupunguza vitendo hivyo.

Alifahamisha kwamba huruma ambayo wanawaonea waume zao ambao ni wabakaji haikubaliki hasa katika suala zima la kumlinda mtoto na kumpatia haki yake.

“Mimi nakuwa nawashangaa sana kinamama wenzangu, baba anafika kumfanyia udhalilishaji mtoto wako ambae umemzaa halafu unasema unaogopa kumpeleka katika vyombo vya sheria kwa kuhofia kuachwa, hili munolifanya sio jambo la haki na tutaenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu juu ya malezi na haki za watoto wetu”, alisema.

Sambamba na hayo wanaharakati hao waliwaomba wazazi na walezi kuwa karibu sana na watoto wao katika kipindi hichi cha mikutano ya kampeni, ambapo kumekuwepo na udhalilishaji mkubwa wa jinsia.

Walisema kuwa katika kipindi hichi vijana hasa watoto wa kike wamekuwa wakivaa nguo za ajabu ajabu ambazo mwisho wake huenda ikapelekea kufanyiwa udhalilishaji.

 “Kipindi hichi ambacho tunaenbda nacho, tuna mikutano ya kampeni ya vyama mbali mbali, watoto wetu sasa hivi wamekuwa wakitumia vibaya mikutano kwa kutoka katika majumba yao wakiwa wamevaa mavazi ambayo si yakuridhisha”, alisema.

Alisema kuwa mbali na kuvaa mavazi lakini hata mida ambazo wanarudi zinakuwa sio rafiki kwao, hali ambayo kama wazazi wnapaswa kuzingatia hilo kwani mambo ambayo huyafanya wakiwa majumbani na ndio hayo ambayo huyafanya katika mikutano hiyo.

“Kwa hiyo tunachosisitizana jamani, hichi kipindi tulichonacho sasa hivi ni kigumu kwa hivyo tuwe nao watoto wetu, lakini pia tuwe na uangalifu nao na ikiwezekana mtoto kama ushamuhisi anakuelekea sivyo bora usimruhusu kwa ajili ya kulinda maslahi yake”, alisema.

Hata hivyo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ( TAMWA Zanzibar), kiko mstari wa mbele kuona matendo ya udhalilishaji yanapunguwa.

TAMWA Zanzibar inasikitishwa kuendelea kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji nchini kote ambavyo vinashamiri kila siku na vinasababisha kuleta hofu na madhara ya kila hali kwa watu wanyonge hasa wanawake na watoto.

Katika kuhakikisha matendo hayo yanapunguwa au kuondoka kabisa TAMWA kupitia mradi wa Jukwaa la Kihabari la kumaliza udhalilishaji (Media Platform), ambao unajumuisha wilaya nne za Zanzibar ikiwemo Wilaya ya Wete, Mkoani, Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja.

Katika mradi huo TAMWA imekuwa ikishirikiana na kamati maalumu ambazo zimeundwa ili kufatilia vitendo hivyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kupambana na ukatili wa kijinsia Unguja na Pemba kwa kipindi cha miezi sita Januari hadi Juni, 2020 matukio 108 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa  katika shehia mbali mbali.

Kati ya matukio hayo, matukio 51 yameripotiwa kuwa ni vitendo vya ubakaji wa watoto chini ya miaka 18, idadi ambayo ni kubwa na inaonesha wazi kwamba bado matendo hayo yanaendelea kufanyika katika jamii.