CAIRO, Misri

TIMU ya Al Ahly ya Misri imeweka hai matumaini ya kutwaa taji la tisa la Ligi ya Mabingwa Afrika na la kwanza kwao tangu mwaka 2013, baada ya kuifunga Wydad Club Athletic ya Morocco mabao 3-1 kwenye mchezo wa marudiano wa nusu fainali uwanja wa kimataifa wa Cairo usiku wa jana.

Mabao ya wenyeji hao jana yalifungwa na Marwan Mohsen dakika ya tano, Hussein Elshahat dakika ya 26 na Yasser Ahmed Ibrahim dakika ya 59, wakati bao la kufutia machozi la Wydad lilifungwa na mtokea benchi Zouheir El Moutaraji dakika ya 82.

Kwa matokeo hayo, Ahly inayofundishwa na Pitso Mosimane kutoka Afrika Kusini, inaingia fainali kwa ushindi wa jumla wa 5-1 kufuatia ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Oktoba 17 Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca.

Ushindi huo unatanua rekodi ya Al Ahly kutofungwa kwenye mechi za nyumbani za Ligi ya Mabingwa hadi kufika 28, wakiwa wameshinda mechi 17 mfululizo nyumbani, ambayo ni idadi kubwa zaidi kihistoria kwenye michuano hiyo.

Na ilikuwa siku njema kwa kocha wa klabu hiyo, Mosimane baada ya mapema Alhamisi kushinda tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) baada ya kuiongoza klabu yake ya zamani, Mamelodi Sundowns kutwaa taji hilo kabla hajahamia Ahly.