CAIRO, Misri
MIAMBA ya Misri, Al Ahly, imeitandika Wydad Casablanca 3-1 na kusonga mbele kwa jumla ya 5-1 na kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mara tu baada ya pambano kuanza, mshambuliaji wa Wydad, Kazadi Kasengu alifanya jitihada kwa kupiga shuti la mbali, lakini, lilitoka nje. Dakika tatu tu baadaye, Marwan Mohsen alijibu kwa kufunga goli.


Goli hilo awali lilikataliwa kwa kuotea, lakini, baada ya kushauriana na VAR, mwamuzi alibatilisha uamuzi huo.
Mashetani Wekundu walishikilia utawala wao katika kipindi chote cha kwanza. Dakika ya 10, Junior Ajayi alipiga shuti kali, lakini, kipa wa Wydad alifanikiwa kuliokoa.
Dakika ya 24, Afsha alikuwa na nafasi ya kuongeza bao mara mbili lakini jaribio lake lilipita juu ya mwamba.


Dakika chache baadaye, Hussein El-Shahat alitumia vyema pasi ya Aliou Dieng, akitembea kwa ustadi kupita safu ya ulinzi kabla ya kucheka na nyavu.
Meneja wa Ahly, Pitso Mosimane, alisema, amefurahishwa na ushindi huo, lakini, anaamini, lazima waanze haraka kujiandaa na mchezo wa fainali.


Ahly imefuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya CAF kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2017-2018, ambapo walishindwa na Esperance Sportive de Tunis.
Chini ya Mosimane, wekundu hao wamepata ushindi mara mbili dhidi ya Wydad Casablanca kwenye nusu fainali 2-0 ugenini na 3-1 nyumbani.


Licha ya matokeo mazuri, meneja huyo raia wa Afrika Kusini anaamini kwamba wanapaswa kuanza kujiandaa kwa fainali.
“Tulifanya vizuri katika michezo ya nyumbani na ugenini dhidi ya Wydad,” alisema Mosimane.
Tulicheza vizuri kwenye mchezo wa kwanza lakini bado hatujafikia kiwango ninachotamani, pia pasi zetu hazikuwa za uhakika. (Goal).