MOGADISHU, SOMALIA

KUNDI linalohusishwa na vitendo vya kigaidi nchini Somalia la Al Shaabab, limeripotiwa kuingiza kipato cha dola milioni 13 kati ya mwezi Disemba mwaka jana Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, imeeleza kuwa kundi hilo la kigaidi limeingiza kiasi hicho cha fedha kutoka na kuwatoza wananchi kodi kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo ilileza kuwa pamoja na kundi hilo la kigaidi kuekewa vikwazo vya kifedha, limevumbua njia hiyo ya kupata fedha ambapo wanalazimisha kulipwa kodi kwa kutumia vitisho.

Taarifa hiyo ilieleza wanachama wa Al Shaabab wanakusanya fedha kwenye mabanki ya Somalia na kuchukua fedha za kodi kwa baadhi ya wafanyabishara kwenye baadhi ya majimbo ya nchi hiyo.

Ijumaa iliyopita jeshi la Kenya (KDF), lilifanya maadhimisho ya miaka 10 tangu ililipoingia nchini Somalia kwa ajili ya kupambana na kundi hilo la kigaidi.

Jeshi la Kenya lilifikiri kwamba linaweza kuchukua muda miezi michache katika kabiliana na kundi la Al Shaabab, hata hivyo mambo yamekuwa magumu ambapo miaka 10 imetimia jeshi hilo halijaweza kuwatokomeza Al Shaabab.

Waziri wa ulinzi wa Kenya, Monica Juma alisema Kenya haijafirikia kuondosha vikosi vyake nchini humo na kwamba itafanya hivyo baada ya kuliona jeshi la Somalia likiwa na nguvu ya kulinda mipaka yake.

“Al Shaabab bado tishio kubwa nashauri Amisom iendelee kusaidia kuvipa nguvu vikosi vya Somalia ili visimame wenyewe katika kukabiliana na kundi hilo hatari”, alisema waziri huyo.