NA KHAMISUU ABDALLAH

MBAO nne mali ya Tip Tip House, alizodaiwa kuiba Abass Patrick Kisaka, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 28 mkaazi wa Forodhani wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu, Nazrat Suleiman na kusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai.

Alidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la wizi kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) na 258 vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Koplo Vuai, alidai kuwa mshitakiwa huyo kwa udanganyifu na bila ya kuwa na dai la haki aliiba mbao nne aina ya msaju tatu zikiwa na urefu wa futi tatu na moja ikiwa na urefu wa futi tano zenye thamani ya shilingi 600,000 zikiwa chini ya usimamizi wa Juma Machano Mohammed mali ya Tip Tip House kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo mshitakiwa Abass alidaiwa kulitenda Juni 7, mwaka 2019, saa 12:00 asubuhi hadi Juni 8, mwaka huo majira ya saa 10:00 jioni huko Shangani wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo, aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana yake mwenyewe huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Koplo Vuai, alidai kuwa hana pingamizi ya kupatiwa dhamana kwa mshitakiwa huyo, kwani ni haki yake, lakini pamoja na kujidhamini mwenyewe lakini pia awasilishe kitambulisho kinachotambulika au barua ya Sheha.

Hakimu Nazrat alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3, mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Pia mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 za maandishi.