NA KHAMISUU ABDALLAH

KITENDO cha kukimbia mahakamani kwa muda mrefu kimemsababishia Mahmoud Rajab Mohammed (34) mkaazi wa Miembeni kukamatwa tena na kufikishwa mahakamani.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 26, mwaka huu, baada ya kukamatwa na askari polisi Oktoba 23 mwaka huu majira ya saa 7:00 usiku katika maeneo ya Miembeni.

Akiwa mbele ya hakimu mdhamini wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, Mohammed Subeit, ambapo ndipo kesi yake inaposikilizwa upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Simni Mohammed ulidai mshitakiwa ameshakamatwa na kuletwa mahakamani.

Alidai kuwa, jitihada za kukamatwa kwa mshitakiwa huyo zinatokana na mdhamini aliemchukulia dhamana mahakamani hapo kuamua kujitoa katika dhamana.

Hata hivyo, ulidai kuwa haujapokea shahidi na kuomba kuhairishwa kesi hiyo na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Mohammed Subeit alisema dhamana ya mshitakiwa huyo imefungwa na kuamuru kupelekwa rumande.

Mahakama iliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 9, mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.