NA KHAMISUU ABDALLAH
MWADIN Khatib Hamis (30) mkaazi wa Tomondo ametozwa faini ya shilingi 50,000 katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe baada ya kukubali kosa hilo na kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya kazi katika njia isiyo yake.
Akisoma hukumu mbele ya mshitakiwa Hakimu Nazrat Suleiman, alimtaka mshitakiwa huyo kulipa faini hiyo na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki nne.
Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo.
Hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo na kusomwa na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Salum Ali, ilidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kufanya kazi katika njia isiyoruhusiwa kinyume na kifungu cha 78 sura ya 135 na kiyume na kifungu 205 (2) (a) na kifungu cha 201 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana Oktoba 1, mwaka huu, saa 5:30 mchana huko Benbella akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 950 HZ inayoenda njia 504 akitokea Majestik kuelekea Mkunazini, alipatikana akiwa anafanya kazi katika njia hiyo wakati akiwa anatakiwa apite Makumbusho kuelekea Benbella kitendo ambacho ni kosa kisheria.