NA KHAMISUU ABDALLAH

HAKIMU Asya Abdalla Ali, wa Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe, amemuachia huru, Khamis Ali Juma (38), mkaazi wa Saraevo Unguja, kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha mashahidi.

Akisoma uamuzi wa Mahakama Hakimu Asya, alisema mahakama inafuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 210 na kuamuru mshitakiwa huyo kuachiwa huru na  alitoa haki ya rufaa kwa muda wa siku 30 kwa mtu asieridhika na hukumu hiyo.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na mashitaka mawili tofauti ikiwemo la kuvunja nyumba mchana na kuingia ndani kwa dhamira ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 297 (1) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa Febuari 15, mwaka 2019, saa 11:00 jioni huko Saraevo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alivunja na kuingia ndani ya nyumba anayoishi, Raya Masoud Mohammed, kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kosa la pili alilodaiwa kupatikana nalo mshitakiwa huyo ni wizi kinyume na kifungu cha 267 (1) na 274 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo, aliingia ndani ya nyumba hiyo na kuiba pesa taslim shilingi laki 950,000 mali ya malalamikaji Raya kitendo ambacho ni kosa kisehria.

Kesi hiyo, ilikuwa inasimamiwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nassra Khamis.