NA MARYAM HASSAN

NDUGU wa merehemu Maryam Hemed Juma (60) mkaazi wa Fuoni wamejitokeza katika hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya kuchukua mwili wake kwa mazishi.

Hayo yameelezwa na msemaji wa hospitali ya Mnazimmoja, Hassan Mcha wakati akizungumza na Zanzibarleo.

Alisema marehemu huyo alifariki Oktoba 6 mwaka huu katika hospitali ya Mnazimmoja alipofikishwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mcha alisema Maryam alifikishwa hospitalini hapo Oktoba 5 mwaka huu akiwa na hali mbaya kiafya baada ya kupata ajali alipokuwa amepakiwa katika bodaboda.

Alisema mama huyo alikuwa amepakiwa katika bodaboda nambari za usajili Z 113 KW, ambapo nguo yake iliingia kwenye tairi ya nyuma na kusababisha kuanguka na kupata majeraha mbali mbali katika mwili wake ikiwemo kukatika mguu wa kulia.

Alisema tukio hilo limetokea Oktoba 5 mwaka huu majira ya saa 12:30 za jioni huko Fuoni Maharibiko wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Aidha alisema kwa upande wa dereva wa honda hiyo aliyetambulika kwa jina la Habibu Shaaban Salum (27) mkaazi wa Meli tano bado yupo hospitali anaendelea na matibabu.

Kwa upande wa ndugu wa marehemu Bakari Shehe Bakari (40) mkaazi wa Chuini alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za marehemu huyo.

Alisema marehemu alikwenda kwa mwanawe wa kike anaekaa Fuoni na alipoondoka ndipo alipopatwa na ajali hiyo iliyopelekea kifo chake.

“Kazi ya Mungu haina makosa na hakuna wa kulaumiwa nilichelewa kupata taarifa lakini nilipopata nikaja hospitali na kuutambua mwili wa marehemu hivyo tunakamilisha taratibu tukafanye mazishi”, alisema.