NA HUSNA SHEHA

KIJANA aliyemkashifu mtoto wa miaka 9  ameanza kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka saba baada ya mahakama kumtia hatiani.

 Mshitakiwa huyo ni Juma Haji Ali (25) mkaazi wa Mahonda Muembe mazizi Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, ambae Mahakama ilitia hatiani baada ya kusomewa shitaka hilo na kulikubali kosa bila ya shaka yoyote mbele ya hakimu Faraji Shomari Juma.

Mbali ya adhabu hiyo pia ametakiwa alipe fidia kwa mlalamikaji ya shilingi 1,000,000 ili iwe funzo kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Hata hivyo Mahakama imetoa nafasi ya rufaa kwa kijana huyo endapo hakuridhika na adhabu hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo inaeleza kuwa kitendo cha kukashifu mtoto wa kike ni kosa kinyume na kifungu cha 114 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria yaadhabu sheria ya Zanzibar.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka PP, Khamis Othman, alieleza kuwa kijana huyo alimchukua na kumpeleka ndani ya nyumba yake na kulaza kitandani na kumvua nguo zake za ndani (chupi na suruali ) alizokuwa amevaa mtoto huyo.

Baada ya kufanya hivyo alisema mtuhumiwa huyo alichana kati kati nguo hiyo ya ndani na kuishusha hadi chini ya miguu na kumnyonya sehemu hiyo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.