NA LAILA KEIS

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limemshikilia Msabaha Makame, mkaazi wa Fuoni Mambosasa kwa kosa la kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali Ali Mohammed Juma (45) mkaazi wa Fuoni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akitoa matukio ya wiki kwa waandishi wa habari, huko ofisini kwake Mwembemadema mjini Unguja.

Alisema, mnamo Septemba 28 mwaka huu, majira ya saa 8:30 usiku huko Fuoni, wilaya ya Magharibi ‘B’, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ali Mohammed ambae ni askari wa ulinzi shirikishi wa shehia ya Mambosasa, alishambuliwa wakati akiwa doria na wenziwe kwa kupigwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia maumivu makali kichwani.

Kamanda alisema, chanzo cha tukio hilo ni kwamba, mtuhumiwa alikamatwa kwa kosa la uchimbaji mchanga katika maeneo hayo, na ndipo alipomshambulia muhanga huyo kwa kumpiga kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwa.

Hivyo muathirika anapatiwa matibabu hospitali ya Mnazi mmoja, huku upelelezi wa kesi hiyo unaendelea, na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.