NA KHAMISUU ABDALLAH

KOPLO wa Polisi Vaui Ali Vuai ameiomba mahakama kuiahirisha kesi inayomkabili mshitakiwa Ali Shaaban Mwinyi (50) mkaazi wa Fuoni Michenzani na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.

Mwendesha Mashitaka huyo alitoa ombi hilo baada ya kuwasilisha mashahidi wawili waliotoa ushahidi mahakamani hapo dhidi ya kesi inayomkabili mshitakiwa huyo.

Hakimu Suleiman Jecha Zidi wa mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22 mwaka huu.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kupatikana na kosa la kutoa lugha za vitisho kinyume na kifungu cha 71 (1) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ali alidaiwa kuwa bila ya halali akiwa ameshikilia msumeno na panga alimtishia Ali Issa Sharif, kwa kumwambia kuwa yeye ni mchawi na popote atakampata atamkata kichwa kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Juni 30 mwaka huu saa 1:30 asubuhi huko Fuoni Michenzani wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Mshitakiwa huyo yupo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 50,000 za maandishi na mdhamini mmoja aliyemdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho kinachotambulika