NA KHAMISUU ABALLAH

KITENDO cha kumpiga mwenziwe mchi wa kichwa na kusababisha kupoteza fahamu kimemsababishia kijana wa miaka 25 kufikishwa mahakamani.

Kijana huyo alitambullika   kwa jina Mohammed Ali Ramadhan mkaazi wa Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zaznibar.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Mohammed Subeit, nakusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka DPP Simni Mohammed.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la shambulio la hatari kinyume na kifungu cha 28 cha sheria ya makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2008 sheria za Zaznibar.

Ilidaiwa kuwa Septemba 12, mwaka 2019 saa 1:30 usiku huko Kiembesamaki mshitakiwa huyo alimshambulia kwa hatari, Rajab Kalanje Alfatiri, kwa kumpiga mchi wa kichwa na kupelekea kupoteza fahamu kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitakahilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilikana kuombakupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Akizungumzia suala la kupatiwa dhamana Simni alisema hana pingamizi ikiwa mshitakiwa huyo atawasilisha wadhamini madhubuti watakaomchukulia dhamana mahakamani hapo.

Hakimu Subeit alimtaka mshitakiwa huyo kujihamini mwenyewe kwa shilingi 500,000 za maandishi na kuwasilisha wanadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha pamoja na kuwasilisha barua ya Sheha na kitambulisho cha Mzaznibari Mkaazi.

Mahakama pia iliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.