NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema juhudi za serikali kwa kushirikiana na wananchi na asasi mbali mbali kwa lengo la kudumisha amani, ni utekelezaji wa miongozo ya ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 na ile ya 2020-2025.

Dk. Shein alieleza hayo jana katika uzinduzi wa kongamano la amani kitaifa, lililofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo Tunguu mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema CCM itaendelea kuhubiri umoja, mshikamano, kupinga ubaguzi wa aina zote na kuliweka suala la kulinda na kudumisha amani kuwa kipaumbele chake katika ilani zilizopita na zitakazokuja.

Alisema Chama hicho kimeielekeza serikali kuendeleza jitihada za kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa amani, umoja na mshikamano ili kujenga mazingira ya kuaminiana, kuvumiliana na kushirikiana katika masuala ya kijamii.

Aidha, alisema ilani ina maelekezo kwa serikali kuendelea kupiga vita na kudhibiti vitendo vya ubaguzi vinavyojitokeza katika sehemu za utoaji huduma za kiuchumi, kisiasa na kijamii miongoni mwa wananchi.

Alisema kongamano hilo ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuzingatia kuwa maudhui yake yanahusiana na wajibu wa serikali wa kulinda amani na usalama kama ilivyoelezwa ndani ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi nchi nyingi duniani hukumbwa na majaribio yenye kuashiria uvunjifu wa amani, ambapo baadhi yake hushindwa kudhibiti matokeo hayo na kupata athari mbali mbali, ikiwemo za kiuchumi.

Aidha, alisema athari nyingine zinazopatikana kutokana na uvunjifu wa amani ni kwa baadhi ya vyama vya siasa kufanya kampeni zenye kuwagawa watu kwa misingi ya dini zao, makabila, uwezo au sehemu wanazotoka.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa mashirikiano waliyompa katika kulinda na kudumisha amani ya nchi na kusema juhudi hizo zimewezesha kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia sekta za kuchumi na kijamii.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kutafakari na kuepuka makosa ya kuwachagua viongozi wasio na dhamira ya kuendeleza umoja na mshikamano wa wazanzibari.