KATIKA nchi inaamini misingi ya kidemokrasi na utawala bora kama zanzibar, kila mtu ana haki ya kushiriki kwenye masuala ya siasa bila kuekewa vipingamizi visivyokidhi taratibu za kisheria.
Kama tunavyoelewa Oktoba 28 watanzania tunatarajia kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi watakao watumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Tukiwa kama wapenda amani tuna matumaini makubwa kwamba tutavuka salama katika uchaguzi huo ili matukio yasiyo ya kufurahisha kama tunavyoyashuhudia katika nchi za wenzetu yanatokea baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Takriban kila siku ipitayo, kumekuwa kukisikika kauli za kuhimiza amani nchini kwa kuwataka wanasiasa wasipandikize mbegu mbaya kwa matamshi yanayoashiria uvunjifu wa tunu yetu ya amani na hivyo kuiingiza nchi katika vurugu na mfarakano.
Uchaguzi utakuja na kupita, lakini nchi itabakia na ni lazima sote kwa pamoja tuhakikishe hatumpi nafasi Ibilisi apenye katika nyoyo na akili zetu kufanya yatakayomfurahisha yeye.
Tumuombe Mungu sana na kwa dhamira ya kweli ili uchaguzi na matokeo ya uchaguzi yasiharibu hali tulivu ya kisiasa iliyopo nchini na kutuachia ombwe litakalotupa wakati mgumu kuliondoa.
Kauli zinazosikika kutoka vinywani mwa baadhi ya wanasiasa wa vyama tofauti wakiungwa mkono na wafuasi wao, si za kupigiwa makofi kwani zinalenga kuturejesha kwenye siasa za chuki, uhasama na ubaguzi ambazo tulikwisha kuzizika na kurejesha umoja, mshikamano na upendo.
Ni busara sana na kwa hili tunakozesha wa msisitizo kuwa Zanzibar haihitaji kurudi tena katika siasa za mtengano, uhasama na kutoshirikiana kwenye mambo ya kijamii na kimaendeleo hata kunyimana huduma kama ilivyowahi kutokezea huko nyuma.
Ni dhahiri kuwa, shetani maluuni hafurahi sanakuona ndugu na watu wanaoishi kwa maelewano na mapenzi wanadumu katika hali hiyo isiyopendeza.
Umefika wakati wazanzibari tujiulize zaidi ya mara moja kabla hatujaamua kuvurugana, hivi tulipata faida gani zaidi ya maumivu kwa mambo maovu yaliyotokea baada vipindi vya chaguzi za miaka iliyotangulia.