NA TATU MAKAME

MAHAKAMA ya Mkoa wa Vuga, itampandisha tena kizimbani Oktoba 13 mwaka huu kijana wa miaka 15 anaekabiliwa na kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 jina linahifadhiwa.

Anaetarajiwa kupandishwa mahakamani ni Mohamed Hamadi Juma (15) mkaazi wa Kwarara Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, ambapo Mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 2018 kwa siku na nyakati tofauti, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka  kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ahmed Mohamed Mbele ya Hakimu Valantina Katema, kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) na kifungu cha 109 (1)  cha sheria namba 6 ya mwaka  2018  sheria ya Zanzibar .

Hata hivyo, mshitakiwa huyo baada ya kusomewa kosa hilo alipewa nafasi ya kujidhamini kwa kusaini bondi ya shilingi 500,000  na awe na wadhamini wawili wenye kusaini dhamana  ya shilingi 1,000,000 kila mmoja na awe na kitambulisho cha mzanzibari mkaazi, pamoja na barua za sheha .

Hata hivyo, mshitakiwa huyo, alitimiza masharti hayo na yuko nje kwa dhamana hadi Oktoba 13, mwaka huu kesi yake itakaposikilizwa tena.