NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya mwanzo Mwanakwerekwe imeiahirisha kesi inayomkabili mshitakiwa Suleiman Hassan Salum (28) mkaazi wa Kianga hadi Novemba 3, mwaka huu.

Hakimu Omar Suleiman Khamis, aliiahirisha kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Time Said, kuiomba mahakama kuhairishwa kesi hiyo na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mshitakiwa huyo anakabiliwa na shitaka la shambulio la kuumiza mwili kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa bila ya halali alimshambulia Haji Othman Mkuu, kwa kumpiga mabapa ya mapanga katika mikono yake na kumsababishia kupata maumivu mwilini mwake.

Koplo Time, alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 5, mwaka huu saa 2:00 asubuhi huko Kianga wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana.

Hakimu Omar, alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 za maandishi na kuwasilisha mdhamini mmoja atakaemdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho chochote kinachotambulika.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo kesi yake itakapofikishwa tena kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.