NA MARYAM HASSAN

JESHI la polisi mkoa wa Kusini Unguja limempandisha katika mahakama ya mkoa Mwera, Sabrina Bakari Khamis (26) mkaazi wa Bwejuu kwa kosa la shambulio la hatari.

Sabrina alipanda mahakamani hapo mbele ya Hakimu Said Hemed Khalfan na kusomewa shitaka lake na wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Ayoub Nassor.

Ilidaiwa mahakamani  hapo kwamba mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 6 mwaka jana majira ya saa 7:40 za usiku huko Bwejuu wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kumshambulia Salma kwa kumpiga chupa ya kichwa kitendo ambacho kimepelekea kumsababishia maumivu mahakali mwilini mwake.

Baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana jambo ambalo lilikubaliwa mahakamani hapo.

Mshitakiwa alitakiwa kusaini bondi ya shilingi 50, 000 pamoja na wadhamini wawili ambao wasaini kima hicho hicho, huku wakiwasilisha kopi ya kitambulisho cha mzanzibar pamoja na barua ya Sheha wa shehiya anayoishi.

Baada ya kupewa masharti hayo mshitakiwa huyo alitekeleza hivyo yupo nje kwa dhamana hadi Novemba 26 mwaka huu kesi yake itapoanza kusilizwa ushahidi.