NA KHAMISUU ABDALLAH

DHAMANA aliyopewa mshitakiwa Ratibu Ashkina Juma ya kujidhamini mweyewe kwa shilingi 500,000 za maandishi na wadhamini wawili watakaomdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha imemshinda na kupelekwa rumande.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 18 mkaazi wa Bububu aliomba dhamana hiyo katika mahakama ya wilaya mwanakwerekwe baada ya kukataa kosa lake la kujipatikana na dawa za kulevya.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nassra Khamis kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na nyingo nane za majani makavu kila kimoja kimezongwa kwa karatasi ya kaki na nyengine ambazo ni dawa za kulevya aina ya bangi.

Mwendesha Mashitaka Nassra alidai kuwa dawa hizo zilikuwa na uzito wa gram 7.353g ambazo ni dawa za kulevya kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Disemba 7 mwaka huu saa 2:15 usiku huko Mtoni wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa ndipo upande wa mashitaka ulipoddai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.

Mahakama ilikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 4 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.