NA MARYAM HASSAN

MSHITAKIWA Anwar Ahmad Ashraka (22) mkaazi wa Fuoni Kibondeni, amerudishwa tena rumande baada ya mkemia kushindwa kufika mahakamani na kupelekea kesi yake kuahirishwa hadi Oktoba 19 mwaka huu.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mkoa Mwera ambapo alishitakiwa kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin.

Kwa mujibu wa maelezo ya hati ya mashitaka mshitakiwa alipatikana na vijiwe 14, vinavyosadikiwa ni dawa za kulevya vyenye uzito wa gramu 1.089 vimemlaza rumande mshitakiwa.

Mshitakiwa huyo pia alipatikana na kete 13 zenye uzito wa gramu 0.574 vyote kwa pamoja vikiwa ni dawa za kulevya aina ya Heroin, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo, anadaiwa kutenda Machi 9, mwaka jana majira ya saa 11:30 za jioni huko Jumbi Bango la Mkoa wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Kikao kilichopita mshitakiwa huyo alipingwa kupewa dhamana na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Safia Serembe.

Pingamizi hizo alizitoa mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfan wa mahakama ya mkoa Mwera ambae nae alikubaliana na upande wa mashitaka juu ya kutompa dhamana mshitakiwa huyo.

Hivyo Hakimu Saidi, aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 19 mwaka huu, kwa ajili kusikilizwa ushahidi na kuamuru mshitakiwa abaki rumande.